Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akizindua Taasisi ya Iyanna Foundation Novemba 26, 2021 jijini Arusha inayojishughulisha na kutoa elimu kwa wanafunzi wa kike na wa kiume kuhusu stadi za maisha ikiwemo kujilinda dhidi ya tatizo la mimba za utotoni na athari za matumizi ya mada ya madawa ya kulevya katika maisha yao.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akiongea na wageni waalikwa wakati wa harambee ya kuchangia Taasisi ya Iyanna Foundation Novemba 26, 2021 jijini Arusha ili iweze kufundisha wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu stadi za maisha ikiwemo kujilinda dhidi ya mimba za utotoni na athari za matumizi ya madawa ya kulevya katika maisha yao.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akiongea na wanamichezo Novemba 26, 2021 katika viwanja vya Nagrenaro Complex jijini Arusha wakati wa bonanza lililoandaliwa na Taasisi ya Iyanna Foundation ambapo wanafunzi walipata wasaa wa kufundishwa stadi za maisha ikiwemo kujilinda dhidi ya mimba za utotoni na athari za matumizi ya madawa ya kulevya katika maisha yao.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Iyanna Foundation Prisca Lema akiongea na wageni waalikwa (hawapo pichani) wakati wa harambee ya kuimarisha taasisi hiyo ili iweze kuendelea kuwahudumia vijana wanaoishi katika mazingira magumu na kuwapa elimu ya stadi za maisha ikiwemo kujilinda dhidi ya mimba za utotoni na athari za matumizi ya madawa ya kulevya katika maisha yao.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akikabidhi kombe kwa timu ya mpira wa miguu kwa wasichana kutoka shule sekondari Olasiti ambao wameibuka mabingwa kwa kuwafunga wenzao kutoka shule ya sekondari Kimaseki kwa jumla ya mabao 2-0. Mchezo huo ulifanyika Novemba 26, 2021 katika uwanja wa Ngarenaro Complex jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akikabidhi kombe kwa timu ya wavulana kutoka Arusha Youth Academy ikiwatandika bila huruma wenzao wa Kijenge Youth Academy kwa jumla ya mabao 2-0. Mchezo huo ulifanyika Novemba 26, 2021 katika uwanja wa Ngarenaro Complex jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul (kulia) akipokea cheti cha shukrani kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Iyanna Foundation Prisca Lema (katikati) wakati Bonanza la michezo kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari lililoandaliwa na taasisi hiyo Novemba 26, jijini Arusha. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Iyanna Foundation Irene Ndossi.
………………………………………………………….
Na Eleuteri Mangi, WUSM-Arusha
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul ameviagiza Vyama vya Michezo pamoja na Maafisa Michezo nchini washiriki mashindano yanayoandaliwa na wadau wa michezo na kutoe elimu ya michezo na utaalamu wao ili michezo hiyo iwe na manufaa kwa wachezaji na taifa kwa ujumla.
Naibu Waziri Gekul ametoa agizo hilo Novemba 26, 2021 jijini Arusha wakati akizindua Taasisi ya Iyanna Foundation ya jijini humo inayojishughlisha na kutoa elimu kwa wanafunzi wa kike kuhusu stadi za maisha ikiwemo kujilinda dhidi ya tatizo la mimba za utotoni.
Uzinduzi huo umeendana pia na mshindano ya michezo ya mpira wa miguu kwa wanafunzi wa kike na wa kiume, mchezo wa kamba kwa wanafunzi wa kike na kiume, mchezo wa kurusha yai kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za jijini humo.
“Kama mdau yeyote anaandaa mashindano ya michezo yeyote ikiwa mpira wa miguu, netiboli, riadha wawajulishe Maafisa Michezo, TFF, Cheneta, chama riadha na mashirikisho mengine waje kwenye mashindano hayo wajionee vipaji vya wanamichezo waviendeleze visipotee. Hawa ndiyo wachezaji watarajiwa wa timu za taifa, timu za taifa ziwe na wachezaji wa damu changa” amesma Naibu Waziri Gekul.
Mhe. Gekul amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Mpango pamoja na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wanapigania sana sekta ya michezo nchini iwanufaishe vijana na wadau wake kwa kuwa michezo ni chanzo muhimu cha ajira kwa vijana wengi na ni chanzo cha kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.
“Rais ameagiza mwaka huu tuanzishe Taifa Cup, Wizara kwa kushirikiana na wadau wa michezo inaratibu mashindano haya na yatafanyika mwezi Desemba mwaka huu, natumia fursa hii wilaya na mikoa muandae timu zenu zishiriki mashindano haya kwa kuleta timu ili kuongeza ushinani na kupata wachezaji bora ambao wataweza kuchezea timu za taifa” amesema Mhe. Gekul.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara inayosimamia michezo nchini imeanza kukusimamia Mashindano ya Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Shule za Sekondari (UMISSETA) nchi ili kuendelea kuibua vipaji vya wanamichezo na kuviendeleza hatua inayosaidias kuwa na timu imara za taifa ambazo Serikali imeanza kuzisimamia zinapokuwa kwenye mashindano ya kimataifa.
Katika kuhakikisha michezo inakuwa na tija nchini, Mhe. Gekul amewahimiza Maafisa michezo kuhakikisha wilaya zote nchini watu wanafanya mazoezi kuanzia mitaa, vijiji, kata, wilaya n ahata mikoa ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanapoteza nguvu kazi ya taifa kuanzia watoto wadogo hadi watu wazima.
Aidha, ameupongeza uongozi wa mkoa wa Arusha na wilaya zake kwa kuwa mstari wa mbele kutafsiri maelekezo ya Serikali kwa vitendo kwa kuwa wanaongoza kwa kufanya mazoezi na mkoa huo umekuwa na mashindano na mabonanza mengi ambayo yanasaidia watu wengi kushiriki hali inayosaidia kuwaondolea shida ya magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na magonjwa mengine.
Kuhusu ugonjwa wa UVIKO-19, Naibu Waziri amesema Watanzania waendelee kuchukua tahadhari kwa kufanya mazoezi ili kujikinga na ugonjwa huo pamoja na kufuata taratibu zote zinazotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hatua itakayowafanya watanzania wawe salama na kuliepusha taifa kupoteza nguvu kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi Iyanna Prisca Lema amesema taasisi yao imejikita kutoa elimu kwa wanafunzi wote wa kiume na wakike kwa shule za msingi (miaka 7-12) na sekondari (miaka 13-25) kuhusu namna ya kujilinda mimba za utotoni pamoja na madawa ya kulevya, magonjwa ya zinaa ikiwemo ukimwi na kuwahimiza na athari zake katika maisha yao huku wakiwahimiza kutumia muda wao vizuri kwenye masomo wakati wote wakiwa shuleni hata nyumbani.
Ameongeza kuwa uzinduzi wa tasasisi yao umekuwa mwanzo mpya na umewatia moyo kwa Serikali kutambua na kuthamini kazi wanayoifanya ya kusimamia maadili na malezi ya watoto wa kiume na wakike ikizingatiwa rika hilo lipo kwenye hatari kubwa zaidi lisiposimamiwa na kuelimishwa ipasayo juu ya makuzi yao na athari za kutokuwa na malezi bora.
Aidha, Mkurugenzi huyo amesema wameamua kuzindua taasisi yako kwa kufungamanisha na tamasha la michezo ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa kuwa wanapenda michezo na ni rahisi kuwapa elimu ya stadi za maisha ili waweze kujiepusha na tabia hatarishi na kufikia malengo yao.
Katika tamasha hilo timu ya mpira wa miguu kwa wasichana kutoka shule sekondari Olasiti wameibuka mabingwa kwa kuwafunga wenzao kutoka shule ya sekondari Kimaseki kwa jumla ya mabao 2-0 huku timu ya wavulana kutoka Arusha Youth Academy ikiwatandika bila huruma wenzao wa Kijenge Youth Academy kwa jumla ya mabao 2-0.
Michezo mingine ilioyochezwa kwenye bonanza hilo ni mchezo wa kuvuta Kamba wa wavulana na wacichana ambapo timu ya wasichana kutoka shule ya sekondari Elerai ndiyo mabingwa kwa kuwavuta wenzao wa shule ya sekondari Njiro kwa mivuto 2-0 huko kwa upande wa wavulana mabingwa ni Sovoi Aacademy ambao waliwavuta wenzao wa Arusha Youth Academy kwa mivuto 2-1 na bonanza kuhitimishwa kwa mchezo wa kurushiana mayai ya kuku na kukimbiza kuku ambapo ushindi wa kufukuza umekwenda kwa shule ya sekondari Elerai huku Salma Yusuph akijipatia kitoweo kwa kumkamata kuku huyo.
Bonanza la michezo linaloandaliwa na taasisi ya Iyana limepangwa kufanyika kila baada ya miezi mitatu ambapo wanaenedela kuongeza wigo wa kushirikisha shulemngingi zaidi ndani ya mkoa wa Arusha na wilaya zake hatua inayosaidia kufikia lengo lao ya kutoa elimu ya stadi za maisha kwa watoto wa kike na wa kiume ili waweze kufikia ndoto zao.
Hatua hiyo pia ya kuigwa kwa kuwa taasisi hiyo inaunga mkono juhudi za kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamguri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa wananchi wanafanya mazoezi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuimarisha afya zao.