*************************************
Dar es Salaam 26 Novemba, 2021
Rais wa Jamhuri ya Uganda Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya Kitaifa kuanzia tarehe 27 Novemba, 2021.
Mhe. Museveni atapokelewa nchini na mwenyeji wake Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na atakagua gwaride la heshima na kupigiwa mizinga 21.
Mara baada ya mapokezi hayo, Mheshimiwa Rais Museveni na Mwenyeji wake Mhe. Samia Suluhu Hassan wataelekea Ikulu ambapo watakuwa na mazungumzo ya faragha na yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi.
Mheshimiwa Rais Museveni na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan watashiriki katika ufunguzi wa kongamano la biashara kati ya Tanzania na Uganda ambalo pamoja na masuala mengine litajikita katika sekta ya mafuta na gesi.
Aidha, Mheshimiwa Rais Museveni atatembelea Bandari ya Dar es Salaam na kukagua mradi unaoendelea wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) katika eneo la Stesheni Kuu.
Pia, Mheshimiwa Rais Museveni atakwenda Wilayani Chato, Mkoani Geita ambapo ataikabidhi rasmi Serikali ya Tanzania Shule ya Msingi iliyojengwa kwa ufadhili wake Wilayani humo na baadaye kuitembelea familia ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mara baada ya shughuli hiyo, Mheshimiwa Rais Museveni atahitimisha ziara yake ya siku tatu nchini na kuagana na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kisha kurejea nchini kwake Uganda.