Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT Askofu Peter Konki,akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kwa niaba ya kamati tendaji ya halmashauri kuu ya Baraza la Maaskofu wa makanisa ya kipentekoste nchini (CPCT)
…………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT Askofu Peter Konki ameiomba Serikali kutunza chakula ambacho kipo katika wakala wa taifa wa hifadhi ya chakula (NFRA)kwa ajili ya tahadhari ya ukame unaendelea sasa nchini.
Ombi hilo amelitoa jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya kamati tendaji ya halmashauri kuu ya Baraza la Maaskofu wa makanisa ya kipentekoste nchini (CPCT)
Askofu Konki amesema kuwa wamekuwa na kikao cha kamati kuu ya halmashauri kuu ya CPCT wajumbe wengine wameshaondoka lakini wao baadhi wamebaki ili kuweza kuongea na waandishi kuhusu jambo hili.
“Hatuwezi kutegemea kulisha watu wetu kwa chakula cha msaada kwani hatufahamu bala la njaa litakuwa na ukubwa wa kiasi gani na huu ukame utadumu hadi lini”amesema Askofu Konki
Amesema kuwa katika maeneo mengi nchini hivi sasa hakuna mvua kabisa hali inayotishia kuwapo na ukame utakao sababisha njaa kutokana na uhaba wa mvua katika msimu huu wa kilimo.
“Wakati kama huu katika maeneo yote nchini ndiyo wananchi huwa wameanza kupanda lakini pia hata majani huwa yameanza kuota lakini mpaka sasa hakuna hata mboga za majani katika maeneo mengi nchini ”amesisitiza Askofu Konki
Aidha, ameishauri serikali kuhamasisha wananchi kuhifadhi chakula walicho nacho majumbani badala ya kukitumia ovyo.
Hata hivyo Askofu Konki amesema kuwa kutokana na hali hiyo Baraza la Maaskofu wa makanisa ya kipentekoste (CPCT) limeandaa maombi maalumu ya kufunga na kuomba kwa muda wa siku 14, kuombea hali hiyo.
“Nitumie fursa hii kuwaalika wanachama wa CPCT na Watanzania kwa ujumla kuungana nasi kushiriki maombi haya yatakayo anza Desemba mosi hadi 14 mwaka huu ili kumuomba mungu atuepushie na hali hii”amesisitiza Askofu Konki