Afisa Mtendaji wa mtaa wa Miambeni kata ya Msamala Manispaa ya Songea Rehema Shadrck kushoto akimuonesha Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge nyaraka mbalimbali za ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa kituo cha afya Msamala kinachojengwa katika eneo la Machinjioni.
Mhandisi wa ujenzi wa Manispaa ya Songea Nicholaus Danda wa pili kulia aliyenyoosha mkono akimuelezea mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge namna ya kazi ya ujenzi wa kituo cha Afya Msamala inavyoendelea vizuri wakati wa ziara ya Mkuu wa mkoa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika manispaa ya Songea,wa kwanza kushoto Mkuu wa wilaya Songea Pololet Mgema.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wa pili kushoto akikagua ujenzi wa msingi wa kituo cha afya Msamala kinachojengwa kwa gharama ya milioni 500 zilizotolewa na Serikali kwa lengo la kusogeza huduma za matibabu kwa wakazi wa kata ya Msamala.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akikagua ubora wa mawe yanayotumika kwenye mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Msamala katika manispaa ya Songea mkoani humo kwa gharama ya Sh.milioni 500 zilizotolewa na Serikali kwa lengo la kusogeza na kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa kata ya Msamala.
…………………………………………………
Na Muhidin Amri,Songea
SERIKALI imetenga Sh.milioni 950 wa ajili ya kujenga vituo viwili vya Afya katika kata ya Msamala na Lilambo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, ikiwa ni mkakati wake wa kusogeza huduma za matibabu kwa wananchi wa kata hizo.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt Frederick Sagamiko, wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo cha Afya Msamala kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.
Alisema, kati ya fedha hizo Sh.milioni 500 zitatumika kujenga kituo cha afya Msamala na Sh.milioni 450 kwa ajili ya kujenga kituo cha afya Lilambo kata ya Lilambo.
Dkt Sagamiko alisema,mradi wa ujenzi wa kituo cha Msamala umeibuliwa na wananchi wenyewe kwa madhumuni ya kupunguza kero ya kutembea umbali mrefu hadi kituo cha afya Mjimwema na Hospitali ya rufaa Songea kufuata matibabu.
Dkt Sagamiko alisema,ujenzi wa mradi huo utahusisha jengo la maabara,upasuaji,jengo la wagonjwa wa n je,wodi ya wanawake,choo cha nje,kichomeo taka,shimo la kondo na shimo la maji taka.
Kwa mujibu wa Dkt Sagamiko,katika utekelezaji wa mradi huo Serikali imetoa Sh.milioni 500 ambapo wananchi wa kata hiyo wamechangia kiasi cha Sh.milioni 2 na unatekelezwa kwa mfumo wa force akaunti na umewezesha wananchi hasa wanaoishi kata hiyo kushiriki katika shughuli za ujenzi na kujipatia kipato.
Dkt Sagamiko alitaja manufaa ya mradi huo mara utakapokamilika ni upatikanaji wa huduma bora ya mama na mtoto na hivyo kupunguza vifo vya akina mama na mtoto kutoka 202 hadi 190 kwa vifo 100,000 kwa mwaka.
Faida nyingine ni upatikanaji wa huduma ya dharura ya upasuaji kwa akina mama wajawazito,kupungua kwa magonjwa ya kuambukiza na yasioambukiza pamoja na wananchi watapa elimu ya lishe,hivyo kupunguza tatizo la utapiamlo kwa Watoto.
Aidha huduma nyingine zitakazo patikana ni chanjo,huduma ya tohara huduma ya upimaji wa VVU/ukimwi na kuzuia maambukizi pamoja na kupunguza mzigo wa wagonjwa uliokuwa unaielemea Hospitali ya mkoa na kituo cha afya Mjimwema.
Pia alisema, katika bajeti ya mwaka 2021/2022 Manispaa hiyo imepanga kutumia Sh.450,000,000.00 ikiwa ni fedha za mapato ya ndani kujenga kituo cha Afya Lilambo na wananchi wamechangia Sh.3,295,000.00 ambapo Sh.160,000,000.00 zimetolewa kutekeleza kazi hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,amemtaka fundi anayesimamia mradi huo kuhakikisha unajengwa kwa viwango na unakamilika kwa wakati ili uweze kuleta tija kwa wananchi ambao walisubiri mradi huo kwa
Alisema,lengo la Serikali ya awamu ya sita ni kuwatatua kero wananchi zilizokuwepo ikiwemo huduma za matibabu,ambapo amewapongeza wananchi wa kata ya Msamala kwa kuibua mradi huo na kushiriki katika shughuli za ujenzi.
Brigedia Jenerali Ibuge alisema,Serikali ya mkoa itakuwa bega kwa bega na wananchi hao na kufuatilia kwa karibu mradi huo ili ukamilike haraka.
Diwani wa kata ya Msamala Michael Mbano alisema, kata ya Msamala ni kubwa na yenye wakazi wengi,hata hivyo kwa muda mrefu haikuwa na huduma zozote za matibabu badala yake wananchi walilazimika kwenda kutibiwa Hospitali ya mkoa na kituo cha Afya Mjimwema.
Mbano ameishukuru Serikali kutoa fedha za ujenzi wa kituo hicho, kwani kitakapo kamilika wananchi wa watapata matibabu karibu na kuwa na afya njema itakayowawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo.