…………………………………………………………………………..
Na. Mwamvua Mwinyi, Pwani
Waziri wa Madini Dotto Biteko amedai kuna baadhi ya watu wamevamia kuchimba madini ya dhahabu katika mto Wami ambapo amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Abdala pamoja na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani Ally Maganga kuhakikisha wachimbaji hao wanaondolewa katika eneo hilo .
Aidha ametoa Rai kwa wamiliki wa migodi ya kuchimba na kuchakata madini ya ujenzi ya kokoto kufuata taratibu na Sheria zilizowekwa na Serikali.
Waziri Biteko amesema hayo, alipotembelea migodi ya Kerai Construction, Even Enterprises, Gulf concrete pamoja na Saint Maria inayojishughulisha na uchimbajii wa madini ya ujenzi ya kokoto iliyopo katika eneo la Lugoba wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Waziri Biteko amesema, Eneo hilo la WAMI ni chanzo cha maji Kama wapo watu hao waondolewe.
Amesema migodi yote inayojishughulisha na uchimbaji wa kokoto katika eneo la Lugoba lazima iandae mpango wa ufungaji wa mgodi baada ya kumaliza uchimbaji (Mining Closure) na uwasilishwe Tume ya Madini kwa ajili ya kusimamia utekelezaji.
Waziri Biteko amezitaka Kampuni zote zinazochimba na kuchakata madini ya ujenzi ya kokoto kuhakikisha wanaandaa mpango wa kuchangia huduma za maendeleo kwa jamii inayowazunguka (CSR) kulingana na vipaumbele vya eneo husika.
“Kuchangia huhuma za maendeleo kwenye maeneo yanayozunguka migodi si jambo la hiari ila ni takwa la kisheria, hivyo niwaombe mkae na Mkurugenzi pamoja na Mkuu wa Wilaya ili mjue vipaumbele vya wilaya katika kuchangia huduma za maendeleo kwa jamii inayowazunguka,” amesema Waziri Biteko.
Pia, Waziri Biteko ametoa wito kwa kampuni zote zinazojishughulisha na uchimbaji wa madini ya ujenzi kuhakikisha wanalipa maduhuli ya serikali kwa kutumia mfumo wa POS ili kupata taarifa sahihi za mauzo na kudhibiti udanganyifu kwenye makusanyo ya mapato ya serikali ambapo wachimbaji wasio waaminifu walikua wakifanya udanganyifu kwenye hati za mauzo ya vitabu.
Kwa upande wake Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es salaam na Pwani Ally Maganga amesema eneo la Lugoba na Msata lina jumla ya Migodi 32 ambapo wa sasa migodi 19 tu ndiyo inayofanya kazi, migodi 13 imesimamisha uzalishaji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo changamoto ya soko hali inayo changiwa na kukosekana kwa miradi ya ujenzi hasa katika jiji la Dar es Salaam.
Maganga amesema, takwimu zinaonesha kuwa uzalishaji wa kokoto kwenye eneo la Lugoba na Msata ni wastani wa tani 2,400,000 hadi tani 2,640,000 kwa mwaka ambapo Serikali hukusanya kiasi cha shilingi bilioni 3.0 hadi bilioni 3.5 kwa mwaka.