Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu,akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo November 24,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022.
…………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
JUMLA ya Wanafunzi 907802 waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka huu wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza ,kati yao wasichana 467967 na wavulana 439835 sawa na asilimia 81.9 ya wanafunzi waliofanya mtihani wakuhitimu elimu ya shule ya msingi mwaka 2021.
Hayo yameelezwa leo Novemba 24,2021 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu wakati akizungumza na Waandishi wa Habari.
Waziri Ummy amesema Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekamilisha zoezi la uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka 2022.
Amesema zoezi hilo limehusisha jumla ya wanafunzi 907,802 wakiwemo Wasichana 467,967 na Wavulana 439,835 ambao ni sawa na asilimia 81.97 ya wanafunzi waliofanya Mtihani wa Kuhitimu Elimu ya Msingi mwaka 2021.
Amesema kati ya waliofaulu na kupangiwa kujiunga na kidato cha kwanza wamo Wanafunzi wenye mahitaji maalum 2,673 sawa na asilimia 0.29 ambao kati yao wavulana ni 1,471 na wasichana 1,202.
Aidha kwa Mwaka 2022 Ongezeko la wanafunzi waliofaulu ni wanafunzi 73932sawa na ongezeko la asilimia 8.87 la wanafunzi waliofaulu tofauti na mwaka 2020walikuwa 833872ambapo kati ya wanafunzi hao wapo Wanafunzi wenye mahitaji maalum 2673 sawa na asilimia0.29kati yao wavulana 1471 na wasicha 1202.
Amesema kwa mwaka 2022 kumekuwa na ongezeko la wanafunzi 73,932 sawa na asilimia 8.87 ya wanafunzi waliofaulu ukilinganisha na mwaka, 2020 ambapo jumla ya wanafunzi 833,872 walifaulu na kupata sifa ya kujiunga na masomo ya Kidato cha Kwanza.
MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA UCHAGUZI WA WANAFUNZI ULIVYOSAIDIA
Aidha,Waziri Ummy amesema : “Mwaka huu kwa mara ya pili uchaguzi wa Wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Kwanza umefanyika kwa kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Uchaguzi wa Wanafunzi (Students Selection-Management Information System),”amesema.
Waziri Ummy amesema mfumo huo umesaidia kupunguza muda unaotumika kwenye uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na masomo ya Kidato cha Kwanza,Kupunguza gharama zinazotumika wakati wa zoezi la uchaguzi na upangaji wa Wanafunzi wa kujiunga na Kidato cha Kwanza.
Amesema pia imesaidia kuongeza ufanisi na uwazi katika uchaguzi wa wanafunzi kwa maana ya kuwa kila mwanafunzi anapangwa kwenye shule kulingana na Mwongozo wa Uchaguzi unavyoelekeza.
WOTE KUANZA MASOMO SIKU MOJA
Waziri Ummy amesema Serikali ya Awamu ya 6 chini ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI ilifanya maandalizi mapema kuhakikisha kuwa wanafunzi wote watakaofaulu Mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka 2021 wanajiunga na Elimu ya Sekondari ifikapo Januari, 2022.
Amesema kutokana na maandalizi hayon wanafunzi wote 907,802 waliofaulu Mtihani wa darasa la saba nchini mwaka 2021 wataanza masomo yao siku moja mara muhula wa masomo utakapoanza.
“Na katika hatua hii natangaza kuwa muhula wa masomo kwa Shule za Msingi na Sekondari zinazomilikiwa na Serikali kwa mwaka 2022 utaanza tarehe 17 Januari 2022,”amesema.
AMSHUKURU RAIS SAMIA
Vilevile,Waziri Ummy amemshukuru Rais Samia kwa kutilia mkazo suala la elimu ya sekondari, na kwa mara ya kwanza aliruhusu jumla ya shilingi bilioni 240 kutumika kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 12,000 nchi nzima.
Amesema kabla ya uamuzi wa mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuongeza vyumba vya madarasa 12,000, shule za serikali za umma zilikuwa na nafasi 430,604 kwa ajili ya kidato cha kwanza ambazo zinaachwa na wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne mwaka 2021.
“Ujenzi huu wa vyumba vipya vya madarasa 12,000 utawezesha upatikanaji wa nafasi za nyongeza 600,000 na hivyo kuwa na jumla ya nafasi 1,030,604 kwa ajili ya kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2022 na hii inaleta ziada ya nafasi 122,802 za kidato cha kwanza kulinganisha na wanafunzi waliofaulu ambao ni 907,802,”amesema.
WANAFUNZI 4,188 WACHAGULIWA KUJIUNGA NA SHULE ZA BWENI
Amesema wanafunzi 4,188 sawa na asilimia 0.46 wamechaguliwa kujiunga na shule za Bweni za Kitaifa, kwa mchanganuo wa Wanafunzi 934 (Wavulana 514 na Wasichana 420) sawa na asilimia 0.1 wamechaguliwa kujiunga na Shule za Sekondari za wanafunzi wenye ufaulu mzuri zaidi.
Vilevile Wanafunzi 1,265 (Wavulana 1,070 na Wasichana 195) sawa na asilimia 0.14 wamechaguliwa kwenda Shule za Sekondari za Ufundi.
Pia,wanafunzi 1,989 (Wav 1,036 na Was 953) sawa na asilimia 0.22 wamechaguliwa kujiunga na Shule za Sekondari za Bweni Kawaida naWanafunzi 903,614 (Wav 437,215 na Was 466,399) sawa na asilimia 99.54 wamechaguliwa kwenda shule za sekondari za kutwa katika maeneo mbalimbali nchini.
WAKUU WA MIKOA NA WILAYA WAPEWA AGIZO
Waziri Ummy ametoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Viongozi na Watendaji wa Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa elimu kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliochaguliwa wanaanza masomo yao mwezi Januari, 2022 bila vikwazo vya aina yoyote ili kutekeleza azma ya Serikali ya utoaji wa Elimumsingi Bila Malipo.
“Jambo hili litafanikiwa endapo kila mmoja kwa nafasi yake atawajibika katika kusimamia ujenzi wa vyumba vya madarasa unaoendelea sasa hivi ili uweze kukamilika kwa wakati kama tulivyojipangia,”amesema.
UJENZI WA MIUNDOMBINU UKAMILIKE KABLA YA KUWAPOKEA WANAFUNZI
Aidha amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha ujenzi wa miundombinu yote kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wa Kidato cha kwanza mwaka 2022 inakamilika kabla au ifikapo tarehe 15 Desemba 2021.
“Kama nilivyoelekeza ili kuhakikisha wanafunzi wote wanaripoti shuleni kwa wakati ifikapo tarehe 15 Januari, 2022 kwa wanafunzi wa Bweni na tarehe 17 Januari, 2022 kwa wanafunzi wanaosoma shule za kutwa,”amesema.
NENO KWA WAZAZI NA WALEZI
Vilevile,amewaagiza , wazazi/walezi na jamii kushirikiana na uongoziwa Wilaya, Halmashauri na Shule, kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliochaguliwa wanaandikishwa, wanahudhuria na kubakia shuleni hadi watakapohitimu Elimu ya Sekondari.