Na. Mwandishi Maalum, Arusha Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC) unaendelea jijini Arusha katika ngazi ya maafisa waandamizi. Mkutano huo ulioanza tarehe 22 Novemba 2021 utahitimishwa na Kikao cha Mawaziri wa Nchi za Jumuiya kitakachofanyika tarehe 29 Novemba 2021. Tanzania ambayo ni mwanachama muasisi wa Jumuiya
hiyo inashiriki kikamilifu katika mkutano huo ambapo Mkurugenzi wa Siasa,
Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi Stephen P. Mbundi anaongoza ujumbe wa Tanzania katika ngazi
ya maafisa waandamizi. Maafisa waandamizi wanaandaa taarifa mbalimbali za
utekelezaji wa shughuli za Mtangamano wa Afrika Mashariki ambazo zitawasilishwa
kwenye ngazi ya Makatibu Wakuu na hatimaye ngazi ya Mawaziri kwa ajili ya kutolea
maamuzi na maelekezo. Waheshimiwa Mawaziri pia watapokea na kupitia
taarifa za utekelezaji wa vyombo na Taasisi za EAC, zikiwemo Bunge la Jumuiya
ya Afrika Mashariki, Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Ofisi ya Katibu
Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kamisheni ya Kiswahili ambayo Makao Makuu
yake yapo Zanzibar na Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Katika jitihada za Tanzania za kukuza lugha ya
Kiswahili duniani, Waheshimiwa Mawaziri watapokea taarifa ya maendeleo ya
mchakato wa kubadilisha sheria na taratibu za EAC ili kuwezesha kuanza rasmi
matumizi ya lugha ya Kiswahili pamoja na
Kifaransa kama ilivyoelekezwa na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki mwezi
Februari 2021. Aidha, Waheshimiwa Mawaziri watapokea taarifa kuhusu mchakato wa
uhakiki wa maombi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwa mwanachama mpya wa
EAC.
|