Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Michezo Bw. Alex Makoye Nkenyenge akizungumza jambo jijini Dar es Salaam katika Mdahalo wa Kitaifa wa kuchambua Utafiti juu ya Ukatili wa kijinsia katika mpira wa miguu kwa wanawake hapa nchini uliondaliwa na Taasisi ya Global Peace Foundation Tanzania kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) chini ya ufadhili wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (Women Fund Tanzania Trust).
Mkurugenzi wa Taasisi ya Global Peace Foundation Tanzania Bi. Martha Nghambi akifafanua jambo katika Mdahalo wa Kitaifa wa kuchambua utafiti juu ya Ukatili wa kijinsia katika mpira wa miguu kwa wanawake.
Mwakilishi wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT Trust) Bi. Bernadetha kafuko akizungumza jambo jijini Dar es Salaam katika Mdahalo wa Kitaifa wa kuchambua utafiti juu ya Ukatili wa kijinsia katika mpira wa miguu kwa wanawake uliondaliwa na Taasisi ya Global Peace Foundation Tanzania kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) chini ya ufadhili wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (Women Fund Tanzania Trust).
Meneja wa Mradi, Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Grobal Peace Foundation Bi. Irene Ishengoma akizungumza jijini Dar es Salaam katika Mdahalo wa Kitaifa wa kuchambua utafiti juu ya Ukatili wa kijinsia katika mpira wa miguu kwa wanawake hapa nchini uliondaliwa na Taasisi ya Global Peace Foundation Tanzania kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) chini ya ufadhili wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (Women Fund Tanzania Trust)
Mwakilishi wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Bw. Boniphance Wambura (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa ZFA Bw. Abdullatif A. Yassin katika Mdahalo wa Kitaifa wa kuchambua utafiti juu ya Ukatili wa kijinsia katika mpira wa miguu kwa wanawake hapa nchini uliondaliwa na Taasisi ya Global Peace Foundation Tanzania kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) chini ya ufadhili wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (Women Fund Tanzania Trust)
**************
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Taasisi mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa michezo wametakiwa kupinga ukatili wa kijinsia katika mchezo wa mpira wa miguu wa wanawake ikiwemo rushwa ya ngono jambo ambalo litasaidia kupiga hatua katika nyanja za kimaendeleo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Taasisi ya Global Peace Foundation Tanzania kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) chini ya ufadhili wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (Women Fund Tanzania Trust) kufanya utafiti juu ya masuala ya Ukatili wa Kijinsia katika soka la wanawake.
Utafiti huo umeonesha asilimia kubwa kuna ukatili wa kijinsia unaofanywa na watu mbalimbali wakiwemo baadhi ya wanajamii, viongozi/wasimamizi wa soka (vilabu, taasisi zinazojihusisha na soka), hata wachezaji wenyewe aidha kwa kujua ama kutokujua.
Mfuko wa Wanawake Tanzania (Women Fund Tanzania Trust)chini ya uongozi imara wa Mkurugenzi Mtendaji, Mama Mary Rusimbi umekuwa mstari wa mbele kufadhili miradi mbalimbali inayolenga kuwawezesha ama kuwajengea uwezo wanawake kugundua talanta na uwezo walionao ndani yao ili wanawake hao wawe sehemu ya mabadiliko chanya katika jamii.
Maono haya ndio yaliwavutia kufadhili utafiti huu ambao lengo lake kuu ni kutokomeza aina zote za ukatili katika mpira wa miguu hasa mpira wa miguu wa wanawake na kuwajengea uwezo wanawake hao kushiriki soka kimafanikio Zaidi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Michezo Bw. Alex Makoye Nkenyenge katika “Mdahalo wa Kitaifa wa kuchambua matokeo utafiti juu ya Ukatili wa kijinsia katika mpira wa miguu wa Wanawake hapa nchini” uliondaliwa na Taasisi ya Global Peace Foundation Tanzania kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) chini ya ufadhili wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (Women Fund Tanzania Trust).
Ukiendeshwa na Bi. Agnes Hanti, Afisa mradi wa maswala ya jinsia kutoka UN women Tanzania, ambao wamekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Global Peace Foundation Tanzania katika kupinga ukatili wa kijinsia katika mpira wa miguu kwa wanawake.
Bw. Nkenyenge amesema kwa sasa kila mmoja anatakiwa kujikita katika kuondoa kiini cha tatizo ili vijana wanawake wapate fursa ya kushiriki mpira wa miguu kwa furaha na amani kwani michezo ni afya na ajira.
Bw. Nkenyenge alikuwa mgeni rasmi katika Mdahalo huo akimwakilisha “Mh. Paulina Gekul Naibu Waziri, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo”, ameeleza kuwa upo unyanyasaji katika soka la wanawake kwani baadhi ya wazazi wamekuwa na tabia ya kuwazui watoto wa kike wasicheze mpira wa miguu.
“Kupitia matokeo ya utafiti na mdahalo huu utatusaidia kupata vitu vizuri ambavyo tutavipeleka katika jamii ili kupata mtazamo mpya ambao utakuwa rafiki katika kulisaidia soka la wanawake kuendelea kupiga hatua” amesema Bw. Nkenyenge.
Amefafanua kuwa serikali inaendelea kutoa ushirikiano katika soka la wanawake kutokana bado wanamchango mkubwa katika michezo, kwani kumbukumbu zinaonyesha mwaka 1965 mwanamke ndiye alikuwa wa kwanza kuleta medani hapa nchini.
Bw. Nkenyenge ametoa wito kwa wadau mbalimbali kufanyia kazi utafiti huo ambao umeonesha changamoto nyingi katika soka la wanawake hapa nchini.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Global Peace Foundation Tanzania Bi. Martha Nghambi, amesema kuwa wameamua kufanya utafiti katika mchezo wa mpira wa miguu wa wanawake ili kuwasaidia waweze kushiriki kwa amani.
Bi. Nghambi amesema kuwa utafiti umefanyika ili kujua kiwango cha ukatili wa kijinsia katika soka la wanawake upo kwa kiasi gani mpaka sasa, kujua mapungufu ya kisera, sheria ndogondogo na miongozo mbalimbali inayoshughulikia masuala ya ukatili katika soka na kuona namna ya kushirikisha wadau wa michezo kwa pamoja kuona namna ya kulitatua tatizo hili kwa maendeleo la soka la Wanawake Tanzania.
Amebainisha kuwa utafiti huo umefanyika katika Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo,”Matokeo kamili ya utafiti huu tutayatoa hivi karibuni kupitia vyombo vya habari na sehemu mbalimbali ili umma waweze kujua kuna ukatili wa jinsia katika sekta ya michezo na waweze kuongeza nguvu katika kupinga ukatili huo” amesema Bi. Nghambi.
Meneja wa Mradi, Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Global Peace Foundation Tanzania Bi. Irene Ishengoma, amesema kuwa “mchezo wa soka kiasili na kiutamaduni unachukuliwa kama mchezo wa kiume, hivyo hata mafanikio ya mchezo huo yanaangaliwa zaidi hata kupewa kipaumbele na kufatiliwa kwao tofauti na wanawake.
Bi. Ishengoma ameeleza kuwa baadhi ya watu wanaamini mwanamke akicheza soka ni kinyume na taratibu na maadili ya kitanzania (uhuni), jambo ambalo linasababisha kikwazo kwa wanawake wengi kushiriki kucheza mpira wa miguu huku wakisahau kuwa soka la Wanawake ni jukwaa la kupaza sauti na kuonesha kuwa Wanawake wanaweza.
“Soka kwa sasa ni fursa kwa kila mtu, ni mahali sahihi kwa mwanamke au msichana kushiriki na kupata mafanikio, hivyo kupitia mradi huu kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii na wachezaji juu ya fursa za ajira/kipato katika sekta ya michezo” amesema Bi. Ishengoma.
Pia, Bi. Ishengoma ameshukuru Wizara ya Michezo, Mashirikisho ya Mpira wa Miguu Tanzania bara na visiwani (TFF na ZFF), Baraza la Michezo la Taifa Tanzania bara na visiwani (BMT na BTMZ), Viongozi wa dini, Vyombo vya Habari, viongozi na wachezaji wa vilabu mbalimbali pamoja na wadau mbalimbali wa michezo waliofanikisha zoezi la ukusanyaji data kwa asilimia kubwa.
Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dkt. M. Lucius, ametoa wito kwa taasisi mbalimbali kuweka mkazo katika kuboresha miongozo na kusimamia soka la wanawake hapa nchini.
Mwakilishi wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT Trust) Bi. Bernadetha kafuko, amesema kuwa michezo ni afya, ajira hivyo wanawake wengi wanatamani kupata fursa kupitia vipaji vyao.
Amesema kuwa rushwa ya ngono inamfanya mwanamke kushindwa kushiriki michezo kwa ajili ya kuonesha kipaji chake cha mpira wa miguu.
“Natamani kuona Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wanalisimamia hilo, pia katika kamati zao za kufanya maamuzi wanakuwepo wakinamama” amesema Bi. Kafuko.
Katibu wa Chama Cha Mpira wa Miguu Wanawake Tanzania (TWFA) Bi. Somoe Ng’itu, amesema kuwa mchezo wa mpira wa miguu kwa wanawake upo na wanaendelea kushiriki ligi mbalimbali kama ilivyo kwa wanaume.
Ameeleza kuwa mpira wa miguu kwa sasa ni ajira na wanawake wengi wamekuwa wakishiriki katika nafasi mbalimbali za soka ikiwemo kusimamia wakiwemo waamuzi na wanaendelea kufanya vizuri.
“Tunajivunia kuona soka la wanawake linachezwa katika ngazi zile zile kama wanaume wanavyocheza, mpira ni ajira, ni taaluma” amesema Bi. Ng’itu.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Bw. Boniphance Wambura amesema kuwa watajitahidi kuyafanyia kazi mawasilisho hasa changamoto zote zilizoonekana katika soka la wanawake.
Bw. Wambura amebainisha kuwa TFF wanasubiri ripoti hiyo ya utafiti katika soka la wanawake kwa ajili ya kuzifanyia kazi changamoto zote zilizoonekana.
Huku Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) Bw. Abdullatif A. Yassin akisisitiza “suala la Wanawake na wasichana wenye vipaji kucheza soka huku wakibakia na uasilia wao wa uanamke ndani na nje ya uwanja”.