Afisa Mikopo Mkuu wa Benki ya NMB Idara ya Biashara, Bw. Daniel Mboto (kushoto) akibadilishana nyaraka na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dk. Venance Mwasse jijini Dar es Salaam, mara baada ya kusaini ushirikiano kibiashara, katika makubaliano hayo NMB itatoa mikopo rafiki kwa wachimbaji wadogowadogo wa madini kwa ajili ya kuwawezesha kununua vifaa vya uchimbaji.
Hafla ya makubaliano kati ya Benki ya NMB na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) iliyofanyika katika ofisi za STAMICO jijini Dar es Salaam ikiendelea. |
Maofisa waandamizi kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) wakifuatilia mazungumzo hayo. |
SHIRIKA la Madini Tanzania (STAMICO) limeingia makubaliano kiushirikiano na Benki ya NMB ili iwasaidiwe wachimbaji na wadau wa sekta ya madini kutoa mikopo rafiki ya ununuzi wa vifaa vya uchimbaji na elimu ya fedha kwa lengo la kuwainua katika shughuli zao.
Wakizungumza katika hafla ya kutiliana saini ya makubaliano ya ushirikiano huo, Afisa Mikopo Mkuu wa Benki ya NMB Idara ya Biashara, Bw. Daniel Mboto amesema NMB itashirikiana na STAMICO kuhakikisha inatambua wahitaji wenye sifa na kuwakopesha mikopo rafiki kwa ajili ya kununulia vifaa vya uchimbaji.
Alisema NMB kwa kushirikiana na wataalamu wa STAMICO watawatambua wachimbaji wadogo wenye uhitaji na kuwapa mikopo hiyo ili iweze kuwainua katika shughuli zao za uchimbaji, huku mikopo ikilenga zaidi uboreshaji vifaa na mitambo ya uchimbaji.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dk. Venance Mwasse akifafanua zaidi alisema lengo la shirika ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wananufaika kikamilifu kwenye shughuli hizo na ndio maana inaendelea kushirikisha wadau taasisi za fedha ili ziweze wakopesha na kuboresha shughuli za uchimbaji kwao.
Aliongeza kuwa STAMICO itaendelea kushirikiana na wadau wengine, katika hatua mbalimbali ili kutoa ushindani wa kibiashara huku ikijikita kuwainua wachimbaji hasa katika uchimbaji wenye tija na uhakika wa wahusika kunufaika na rasilimali hizo.
“Tumejipanga kununua mashine za kuchoronga miamba kila mwaka ili kuhakikisha tunawasaidia wachimbaji wadogo kutambua maeneo yenye tija na uhakika wa kumnufaisha mchimbaji , tofauti na hapo awali walipokuwa wakipotenga nguvu nyingi hata katika maeneo yasio na uhakika wa rasilimali hiyo,” alisema Dk. Mwasse.