Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua mkutano wa 20 wa Taasisi za Fedha nchini utakaofanyika jijini Dodoma, tarehe 25 na 26 Novemba 2021, utakaojadili uimarishaji wa uchumi wa Tanzania kufuatia janga la UVIKO-19.
Mkutano huo, ambao umeandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa Mabenki nchini (TBA), unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki takribani 300 kutoka taasisi za fedha, sekta binafsi, serikali, mashirika ya kimataifa, taasisi za elimu, asasi za kiraia na vyombo vya habari.
Mada nne zitawasilishwa na wataalam waliobobea kutoka ndani na nje ya nchi, ambazo ni:
∙ Ukuaji wa uchumi endelevu wakati na baada ya janga la UVIKO -19: Vipaumbele na sera mbadala;
∙ Kuchochea kasi ya maendeleo ya kidijitali katika kuimarisha ukuaji endelevu wa uchumi;
∙ Sarafu za kidijitali: Uzoefu, vihatarishi na usimamizi; na
∙ Kuongeza mikopo kwa sekta binafsi baada ya janga la UVIKO-19: Wajibu wa Serikali, taasisi za fedha na sekta binafsi.
Mada hizo zimechaguliwa kuendana na hali ya sasa, ambapo uchumi wa dunia unaendelea kuimarika kufuatia athari za janga la UVIKO-19, na kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia za kidijitali na fedha za mtandaoni.
Mikutano ya Taasisi za Fedha ilianzishwa na Benki Kuu ya Tanzania mwaka 1980 na imekuwaiukifanyika kila baada ya miaka miwili. Mkutano wa 19 wa Taasisi za Fedha ulifanyika jijini Dar es Salaam mwezi Novemba 2019.