Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kitandi wilayani Ruangwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipokagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kitandi wilayani Ruangwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye viwanja vya Shule ya Skondari ya Kitandi wilayani Ruangwa kukagua ujenzi wa Shule hiyo
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Safiel Fazael ambaye ni Fundi Mkuu aliyepewa jukumu la kujenga madarasa manne katika Shule ya Sekondari ya Kitandi wilayani Ruangwa wakati alipokagua ujenzi wa Shule hiyo, Novemba 22, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo wilaya ya Ruangwa, hivyo ni lazima fedha hizo zitumike kama ilivyokusudiwa.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameagiza kwamba wenyeviti wote wa kamati za ujenzi wa mradi hiyo ikiwemo ya ujenzi wa vituo vya afya pamoja na shule watoke katika vijiji ambavyo miradi husika inatekelezwa ili kurahisisha usimamizi.
Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Novemba 22, 2021) wakati akikagua ujenzi wa shule ya Sekondari Kitandi iliyoko Kata ya Likunja wilayani Ruangwa, Lindi akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo mkoani Lindi.
Waziri Mkuu amewataka watu wote walioko kwenye kamati zinaosimamia miradi hiyo wawe waadilifu na wahakikishe wanadhibiti vitendo vya wizi katika maeneo yote yanayotekelezwa miradi na ijengwe kwa viwango. “Lazima tuzilinde fedha zilizotolewa na Rais wetu mpendwa.”
Amesema kuwa mpango wa Mheshimiwa Rais Samia ni kuhakikisha watanzania wanapata huduma zote za kijamii ikiwemo Afya, maji, umeme, barabara ili kuwarahisishia kutekeleza shughuli zao “maendeleo haya yote ni kutokana na juhudi za mkuu wa nchi, lazima tumuunge mkono”
“Kiongozi wa nchi ametoa fedha, hatuwezi kuvumilia kuona mtu mzembe kwenye miradi ya Serikali, huu ni ujumbe kwa kamati zote zinazosimamia ujenzi wa miradi nchini. Wananchi wanatajaria kuona miradi hii inakamilika, simamieni miradi na iishe tena kwa viwango, Mheshimiwa Rais Samia anatoa fedha kwa ajili ya miradi hii ya wananchi”
Waziri Mkuu amesema kuwa wajumbe wote wa kamati za ujenzi wa miradi nchini washirikishwe kwenye hatua zote za ujenzi ikiwemo ununuzi wa vifaa vya ujenzi.
Kwa upande wake, Katibu wa Mradi huo Mwalimu Arafa Msuya amesema ujenzi wa shule hiyo mpya ya sekondari ya Kitandi ambayo ni ya bweni itakayosajili watoto wa kike na kiume kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita itapunguza adha ya wanafunzi wa maeneo hayo kutembea umbali mrefu hadi shule ya sekondari ya Likunja.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa imepokea shilingi bilioni moja kutoka Serikali Kuu kupitia mradi wa EP4R kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo unaojumuisha miundombinu ya majengo 16 ambayo ni jengo la utawala, majengo matano yenye jumla ya vyumba 13 vya madarasa.
Miundombinu mingine ni ujenzi wa mabweni manne yakiwemo mawili ya wanafunzi wa kike na mawili ya wanafunzi wa kiume, ujenzi wa nyumba mbili za walimu ambazo ni kila mmoja inauwezo wa kuishi familia mbili, ujenzi wa bwala la chakula na jiko la nje, matundu 30 ya vyoo na ujenzi wa kichomea taka.
Nao, mafundi wanaojenga mradi huo kupitia mfumo wa force account wameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa mradi huo kwa kuwa mbali na kusogeza huduma za jamii karibu na wakazi wa wananchi pia inatoa ajira kwa wananchi wengi hususani wanaoishi katika maeneo ya karibu. Wameahidi kuikamilisha kwa wakati na kwa viwango.