……………………………………………………………….
Mkurugenzi wa bodi ya maji bonde la ziwa nyasa Mhandisi Elice Engelbert ameitaka Jumuiya ya watumia maji mto katewaka kufanya kazi kwa weledi na kutokuzua taharuki kwa wananchi wanapotekeleza majukumu yao bali wawape elimu ya kujua utaratibu wa kutumia vyanzo vya maji bila kufanya uharibifu wowote.
Hayo ameyasema wakati wa uzinduzi wa jumuiya hiyo uliofanyika katika kata ya Lugarawa wilayani Ludewa mkoani Njombe ambayo imehusisha vijiji tisa kutoka katika tarafa mbili ambayo ni tarafa ya Mlangali na Liganga.
Amesema serikali imetumia fedha nyingi katika kuunda jumuiya hiyo hivyo endapo hakutakuwa na badiliko yoyote katika vyanzo vya maji watapaswa kuwajibika.
Chiwaya Nkomola ni afisa maendeleo ya jamii bonde la ziwa nyasa amesema walitoa mafunzo sambamba na kuandaa mpango wa pamoja wa usimamizi wa huduma za maji katika mto ketewaka na kufikia hatua ya kutengeneza katiba.
Ameongeza kuwa baada ya kukamilisha taratibu zote walirudi kwa wananchi ili kutolea maoni rasimu ya katiba na utaratibu wa matumizi ya maji ambapo vijiji vyote tisa vilipata nafasi ya kutoa maoni hayo na baada ya hapo waliweza kupatikana viongozi wa jumuiya hiyo.
Aidha kwa upande wa mgeni rasmi ambaye ni mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsere amewataka wanaotumia maji kwa matumizi mbalimbali kutoka katika mito na vyanzo vinginevyo vinavyotiririsha maji yake katika ziwa nyasa kutunza vyanzo hivyo na kufuata sheria ya kuwa na leseni ya matumizi ya maji hayo.
Sanjari na hilo pia mkurugenzi huyo akiwa na mgeni rasmi ambaye ni mkuu wa wilaya Andrea Tsere pamoja na viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo walizindua katiba ya jumuiya hiyo sambamba na kuwakabidhi vifaa vya kazi pamoja na usafiri wa pikipiki ili kuweza kuyafikia maeneo yote kwa urahisi huku katibu wa jumuiya hiyo akieleza mafanikio waliyofikia kwa kuundwa kwa jumuiya hiyo.