…………………………………………………….
Adeladius Makwega,Mbagala
Novemba 19, 2021 niliamka mapema ili kwenda kutafuta riziki hapa Chamwino Ikulu, kabla sijatoka nyumbani kwangu nilichukua ufunguo wangu na kuwafungulia kuku wangu ambao kwa hakika wananisaidia kama kitoweo na kujipatia kidogo mayai ili kusogeza siku. Hata akija mteja kununua huwa nauza japokuwa kuku wangu ni wachache sana. Nililisogelea banda hilo na kukuta kuku hao wakiwa wanasinzia.
Basi niliwafungulia kuku hao wakienyeji na kuelekea kuganga njaa. Jioni wakati narudi nilikutana na mama mmoja ambaye ni jirani yangu akiwa amejitwika kuni kichwani, nilimuuliza vipi tena jumamosi hii na kuni kichwani? mama huyu alinijibu kuwa kuni hizo ambazo ziliambatana na kijifurushi kidogo, akisema kesho jumapili Novemba 20, 2021 anakuja askofu kwa hiyo hayo ni maandalizi ya kumpokea Baba Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Centra Tanganyika ambaye jina lake sikulifahamu.
Mama huyu ambaye ni mfugaji wa kuku nilijaribu kumuuliza vipi mwezangu kuhusu kuku wako wanasinziasinzia kama wangu? alinijibu kuwa huo ugonjwa upo na nikifanya utani kuku wangu watapukutika na nitakula wa chuya. Niimwambia kuwa wangu wanasinziasinzia na nimeshapoteza kuku saba sasa kwa ugonjwa huo.
Jirani huyu alinielekeza dawa za asili za ugonjwa huo nisage majani ya shubiri niwawekee kuku hawa katika maji na kweli nilifanya hivyo
Jibu hilo lilinipa picha kuwa ugonjwa huo si kwangu hata kwake upo. Mama huyu kwa kuwa alikuwa na mzigo wa kuni nilimwacha aende zake akafanye maandalizi ya kumpokea askofu wake. Novemba 21, 2021 nilikuta kuku wengine kadhaa wakiwa wamekufa, asubuhi hii niliwauliza majirani wengine wakasema kuwa ugonjwa huo ukiingia wacha tu watakufa wengi lakini wapo watakaobaki.
Nikiwa natafakari hilo mama huyu jirani yangu ambaye nilikutana naye siku iliyotangulia aliyekuwa na kuni kichwani aliniambia kuwa anauza njugu mawe debe mbili, nikamuuliza za aina gani alinijibu za maganda debe ni shilingi 8000/-maana yake kwa debe mbili ni shiilingi 16,000/-na shilingi 2000/-ya kuzimenya. Jumla 18,000/- nikaomba aniwekee ili niweze kulipa baadae akasema sawa. Debe hizo mbili zikimenywa unapata kati ya kilo 12-13, ambapo kwa bei ya dukani kilomoja ni shilingi 2000/- sawa na shilingi 26,000/-
Mama huyu kwa kuwa nilimuuliza habari ya ugonjwa wa kuku aliniuliza habari ya kuku wangu inaendeleaje/ nilimwambia kuwa kuku wangu sasa wamepaki 6 wanakufa kila siku pengine ikifika jumapili ijayo banda langu linaweza kuwa tupu kwa kuku wote kufa. Nikamtania, mdala(bibi) nitakuja kuomba mbegu ya kuku wa kufuga! mama huyu alijibu sawa jirani.
Hiyo ndiyo kawaida ya kupeana kuku wa kufuga hata mie wakifa kwangu nitakuja kwako kuomba mbegu angalau kuwa na kuku hata wa dawa, alisema mama huyu. Maana ukienda kwa mganga angalau kuwa na kuku huyo siyo tena unaenda kuazima kuku kwa mwingine hata huo ugonjwa hauwezi kupona.
Mama huyu aliniambia kuwa ugonjwa huu wa kuku ni wa miaka mingi sana, sisi tunazaliwa, tunakuwa hadi wali, tunaolewa, hadi sasa tunajukuu huu ugonjwa upo, jirani !
“Sisi tulitolewa katika makaazi yetu ya asili ya mababu kuja kukaa hapa Chamwino tukiambiwa jamani njoni mkae pamoja, mkikaa pamoja tutaleta dawa za Sulua, Polio, Kifaduru, Sotoka, Mdondo, Donda Ndugu, Ndonda Koo na Kipindupindu.”
Tuliambiwa tukikaa pamoja Katika Vijiji vya Ujamaa hakuna binadamu wala mnyama ambaye atakufa kwa mangojwa haya.
Kweli tuliitikia sana tukaja kuishi pamoja katika vijiji vya ujamaa na mie nikaolewa na mwalimu Mnyamwezi kutoka Tabora ambaye alikuja kusomesha shule zetu wakati huo.Vinginevyo ningeolewa na Wagogo wezangu.
“Kweli Sulua na Kifaduru, Polio, Ndonda ndugu, Sotoka , Donda Koo yalikwisha lakini hili la ugonjwa wa Mdondo wa kuku bado lipo tena limezidi sana.”
Mama huyu anasema kuwa wakati wakiwa wakiishi katika makaazi ya familia walikuwa na ng’ombe, mbuzi, kondoo mbwa, paka, bata na kuku, kuku walikuwa wanakufa lakini si wengi kama sasa. Akiamini kuwa ipo siku itapatikana dawa tu.
Kwa umri wa mama huyu ni kati ya miaka 69-80, kwa umri huo ninaweza kusema kati mwaka 1972-1974 wakati wa vijiji vya ujamaa alikuwa mama wa umri wa miaka 24-34. Ndiyo kusema alikuwa mtu mzima akitambua fika kilichokuwa kinafanyika.
Baba yangu mzazi Francis Fidelis Makwega ambaye umri wake unalingana na mama huyu aliwahi kunisimulia kuwa wakati wa ujamaa alifika katika vijijini vya Dodoma katika Oparesheni Vijiji vya Ujamaa ambayo sehemu ya vijiji hivyo vya wilaya ya Dodoma na Mpwawa na wakati huo ambavyo sasa ni sehemu ya wilaya ya Dodoma, Chamwino Kongwa na Mpwapwa.
“NI kweli nilifika maeneo haya ya Wilaya ya Dodoma na Mpwapwa nikitokea Mafinga JKT na kabla ya hapo nilikuwa mkurufunzi wa chuo cha Ualimu Marangu. Nyumbani kwetu kwa wakati huo kulikuwa ni Kilindoni-Mafia, Mkoa wa Pwani. Tulipofika Dodoma tulishiriki zoezi hilo la kuwahamisha wakaazi wa vijiji mbalimbali na vijiji vya ujamaa vikaanza. Kwa hakika Wagogo walitupokea vizuri na walikuwa ni watu waelewa sana.”
Anasema kuwa alipomaliza zoezi hilo wale wote walioshiriki Oparesheni Vijiji vya Ujamaa walimu walipangiwa kazi maeneo jirani na waliposhiriki zoezi hilo akiwamo yeye. Anasema kuwa alipangiwa kazi yeye na dada yake kama walimu katika Wilaya ya Mpwapwa.
Kutambua ukweli wa walivyokuwa wakiwashawishi wananchi kuhamia katika vijiji vya ujamaa nilimuuliza namna walivyokuwa wakifanya, aliniambia kuwa waliwaeleza juu ya mahitaji kama vile shule, zahanati na hata namna ya kupambana na magonjwa ya binadamu na wanyama.
Mzee wangu aliniambia kuwa wakati wa oparesheni Vijiji vya Ujamaa Wagogo waliielewa vizuri sana kutokana na hilo yeye aliamua kuoa hukohuko ugogoni na wala hakuona tija ya kurudi Kilindoni-Mafia au nyumbani kwao kwa asili Mahenge kutafuta mchumba.
Aliongeza kuwa hapo alipotafuta mchumba ndipo tulizaliwa sie. Hapo niligundua kuwa, kumbe hata mimi ni tunda la vijiji vya ujamaa. Mzee huyu aliniambia kuwa hata dada yake aliyeajiriwa Mpwapwa alipata wachumba wawili ambao wote hawakuwa wa kabila moja, lakini nilitaka kujua nani alioa dada huyu wa mzee wangu?
Kwani alinimbiwa kuwa dada huyu alikuwa na wachumba wawili ambao mmoja ni mwalimu na mwingine Hakimu/Mwanasheria. Nikiwa nazungumza naye hayo kwa simu, Gafla simu hiyo ilikatika na mie kumpigia kutokana na gharama za simu yake nilishindwa, lakini akinipigia simu siku nyengine nitamuuliza na msomaji wangu nitakusimulia maana kisa hicho pia kina mengi.
Hoja ya leo ni moja tu, sasa ni miaka 60 Tangayika inatimiza tangu ipate uhuru, wapo Watanzania ambao walishuhudia jitihada kadhaa mara baada ya uhuru na ahadi zilizotolewa ambazo hazijakamilika ikiwamo ya kutokomeza ugonjwa wa huu wa kuku, linaweza kuonekana ni jambo dogo lakini halijatimizwa sasa ni wakati wa kulitatua hilo na wizara husika inapaswa kulifanyikia kazi. Kwani hiyo ni miongoni mwa ahadi zilizotolewa enzi ya Oparesheni Vijiji vya Ujamaa.
0717649257