Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi. Robert Gabriel, akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kilimani wakiwemo walimu wa shule hiyo jana baada ya kukagua ujenzi wa madarasa yanayojengwa kwa fedha za Uviko-19.
Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya Kilimani sekondari,Salvatory Emmanuel, akimwonyesha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel (mwenye skafu), ramani (master plan) ya shule hiyo jana baada ya kukagua ujenzi wa madarasa mawili ya shule hiyo.
*******************************
NA BALTAZAR MASHAKA, Ilemela
WANAFUNZI wa shule za sekondari Kilimani, Bujingwa na Buswelu,katika Manispaa ya Ilemela, wamemshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kutambua upungufu wa miundombinu ya madarasa na kutoa fedha za kujenga vyumba 15,000 nchini.
Walitoa shukrani na pongezi hizo jana mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandis.Robert Gabriel,wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba 11 madarasa kati 97 yanayojengwa wilayani Ilemela.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanafunzi hao Salvatory Emmanuel na Getrudeshose Kessy (Kilimani),Paulina Faustine na Aloys Martin (Bujingwa),Leokadia Aisha Bunu na Sekei Samike (Buswelu), walisema kuwa miundombinu hiyo itasaidia kuondoa msongamano na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Walisema kuwa Rais Samia kwa kuwasaidia kupata madarasa hayo ameonyesha mwanga na uzalendo kwa kujali elimu yao na kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani ambapo walimwahidi kusoma kwa bidii na kufanya vizuri ili watimize ndoto zao.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa mchango wake wa fedha sh. milioni 40 za kujenga vyumba viwili vya madarasa, pia atusaidie kutatua na kufanyia kazi changamoto za Kilimani zilizoanishwa na Mkuu wa Shule,”alisema Emmanuel.
“Mama yetu Samia tunampongeza kwa kutambua changamoto za sekta ya elimu na kuamua kutoa fedha za kujenga madarasa,Kilimani ni sehemu ya kitovu cha taaluma hivyo rai yangu kwa serikali ya mkoa ione namna ya kushirikiana na wadau kujenga hosteli ili kuwawezesha watoto wa kike kupata elimu bora,” alisema Kessy.
Pia Leokadia, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia madarasa hayo yakikamilika,yatapunguza msongamano na yataongeza ari na morali ya wanafunzi kujifunza kwa bidii.
Aidha Samike, alisema serikali kwa kuwajengea miundombinu hiyo ya madarasa imetambua umuhimu wa elimu ya watoto masikini hivyo wanamwombea Rais maisha marefu huku Aisha Bunu akisema Rais Samia kwa kuonyesha kuwajali wanafunzi, watasoma kwa bidii na kufaulu kutokana na kuwezeshwa vyumba vya madarasa.
Awali akiwa Kilimani sekondari Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mhandisi. Gabriel aliwaasa wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuonya wasichanganye mapenzi na masomo, wajiepushe na mimba za utotoni ili wafikie ndoto zao za maisha.
Alisema kila jambo duniani lina kanuni kadhaa za kuzingatia ili kupata mafanikio ni kufanya kazi kwa bidii na nidhamu,pia kwenye elimu ili kufanya vizuri katika masomo ni kusoma kwa bidii ukilala kwa saa 3 unafeli (fail).
“Hakuna njia ya mkato kwenye mafanikio, kumtanguliza Mwenyezi Mungu mbele,kuwa na maisha yenye nidhamu,hivyo ni muda wa kusoma si wakutafuta mchumba,masomo hayachanganywi na mapenzi,someni mtimize ndoto zenu.
Alieleza kuwa watu waliofanikiwa duniani wana nidhamu na kushauri wanafunzi hao kuwa bado ni watoto wadogo hivyo wasome kwa bidii wakitambua kuna nyakati mbalimbali za kupanda na kuvuna, jua na mvua,masika na kiangazi hivyo ni wakati wao wa kusoma.
“Ukilala saa 2 au saa tatu unafeli, ukifika nyumbani jioni fanya kazi za nyumbani na za shule, kama umepewa maswali kabla ya kulala fanya,Jumapili na Jumamosi msome na kabla ya mitihani ya Taifa fanyeni maswali ya mitihani ya miaka mitano nyuma au miaka 10 iliyopita hiyo itasaidia misuli yako ya uelewa iweze kuzoea,hakuna njia fupi kwenye mafanikio,”Mhandisi.Gabriel alisema.
Alishangaa mtoto wa kidato cha kwanza hadi cha nne kupata ujauzito aliyempa ujauzito yupo kidato cha pili, haeleweki leo ana mtoto nani anayemlea, shida anapeleka nyumbani na watoto watakuwepo tu hawaishi “muda wako wa kusoma tumia kusoma ili utimize ndoto yako huu ndio wosia wangu,”alisema.
ssssssssssssss