*************************
Na Abby Nkungu, Singida
JUMLA ya kaya 745 katika halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, hazina vyoo hali inayosababisha wakazi wake kujisaidia kwa majirani, mashambani na vichakani hivyo kuwa hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko; hasa watoto wenye umri chini ya miaka nane.
Takwimu hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmshauri hiyo, Justice Kijazi katika kipindi hiki ambapo Tanzania iliungana na nchi nyingine duniani kote wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya choo Duniani ambayo hufanyika Novemba 19 kila mwaka.
Kijazi alisema kuwa kati ya kaya zaidi ya 69,900 zilizopo katika halmashauri hiyo, 38,544 ndizo zenye vyoo bora, 30,681 zina vyoo vya kawaida visivyokubalika kiafya wakati zingine 745 hazina vyoo.
“Baadhi ya kaya ambazo hazina vyoo na zile zenye vyoo visivyokubalika kulingana na kanuni za afya, kunachangia kuwepo kwa magonjwa mbalimbali ya mlipuko kikiwemo kipindupindu, kuhara, kuhara damu pamoja na homa ya matumbo” alisema na kuongeza;
Waathirika wakubwa wa changamoto hizo ni kundi la watoto ambapo takwimu zinaonesha kuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, jumla ya watu 10,091 waliugua magonjwa hayo kati yao 5,819 yaani zaidi ya nusu wakiwa ni watoto walio chini ya umri wa miaka nane”.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Kijazi alisema kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kuwa na vyoo bora na kutumia Sheria Ndogo za halmashauri kuwabana wanaokaidi.
Alisema kuwa hatua hiyo itaenda pamoja na kusimamia miongozo ya Wizara ya Elimu na Afya ili kuhakikisha kuwa shule zote zinakuwa na vyoo bora kwa ajili ya kulinda afya za watoto wawapo shuleni.
Daktari bingwa Mshauri wa magonjwa ya wanawake na watoto katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida, Dk Suleiman Muttani alisema kuwa vyoo bora shuleni na nyumbani ni muhimu zaidi katika kulinda afya za watoto na jamii kwa ujumla..
“Mtu mzima akibanwa atakwenda kwa jirani au kichani lakini mtoto kama hujamjengea choo, yeye atajisaidia hapo hapo kwenye uwanja nyumbani au kama ni shuleni basi nyuma ya madarasa na ni hatari kwa kuathiri shule nzima au kaya yote kwa magonjwa ya mlipuko” alieleza Dk Muttani.
Hata hivyo baadhi ya wadau wanasema kuwa tatizo ni elimu duni juu ya umuhimu wa vyoo bora, mila potofu na ukosefu wa teknojia rahisi ya ujenzi wa vyoo bora bila kutumia gharama kubwa hasa vijijini.
“Kuna wengine kwa mila na desturi zao wanachukulia choo kuwa ni kitu cha anasa. Yaani atoe 200,000/- au zaidi kujenga choo wakati vichaka vipo, hawawezi…. anaona bora akanywee pombe hiyo hela. Lazima elimu itolewe, watu wajue kinagaubaga kuwa iwapo hawana choo wapo kwenye hatari” alisema Patrick Mdachi Ofisa Maendeleo ya Jamii Mstaafu na mtafiti wa mila na desturi za kabila la Wanyaturu.
Novemba 19 kila mwaka, dunia huadhimisha Siku ya Choo Duniani ili kutoa fursa kwa wanajamii kutathimini juu ya hali ya vyoo, kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora, kuvitumia na kuzungumzia usafi wa mazingira kwa ujumla. Ujumbe wa mwaka huu ukiwa “Tuthamini Vyoo”
Aidha, siku hii huchagiza uchukuaji hatua madhubuti katika kushughulikia janga la Usafi wa Mazingira duniani ili kusaidia kufikia lengo namba 6 la Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDG 6) linalohimiza Usafi wa Mazingira kwa wote ifikapo mwaka 2030.