*******************************
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.Zaidi ya Watanzania 300 wanatarajiwa kupanda Mlima Kilimanjaro kuanzia chini hadi kileleni ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania ambayo itaadhimishwa kitaifa Disemba 9, 2021.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha umma wa Watanzania kupanda Mlima Kilimanjaro leo Novemba 21, Jijini Arusha, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Damasi Ndumbaro amesema tayari watanzania 120 wamethibitisha ushiriki wao.
Amesema kuwa, Mlima Kilimanjaro mbali ya kuwa kivutio kikubwa Afrika na Duniani pia una historia kubwa sana katika nchi ya Tanzania ambayo kila mtanzania anapaswa kuijua na kuwa kumbukizi kwa vizazi na vizazi.
Dkt Ndumbaro amesema Tanapa kwa kushirikiana na kampuni ya utalii Zara Tours Kama waratibu wa ziara hiyo imeamua kutoa fursa hiyo adhimu kwa watanzania ili waweze kujivunia uwepo wa mlima huo nchini.
“Hii ni fursa pekee na adhimu nchini kwa kuwa tunatarajia watu mbalimbali watashiriki kupanda Mlima Kilimanjaro, watapanda sio tu kutalii lakini pia kuadhimisha miaka 60 tangu tulipopata uhuru nchini, hili ni jambo kubwa sana,”anasema.
“Tunatarajia safari ya kupanda mlima Kilimanjaro itaanza Disemba5, 2021 ambapo watakapanda watatumia njia ya Marangu ambayo inachukua takribani watu 120 na baadae tutafungua njia zingine kwa kadiri watu watakavyokuwa wakiongezeka,” amesema Ndumbaro.
Kampuni ya utalii ya Zara ndio mratibu mkuu wa safari hiyo ya kupanda Mlima Kilimanjaro ambapo kwa mujibu wa maafisa wake, kampuni inaouwezo wa kuhudumia idadi kubwa zaidi ya wageni watakaokuwa tayari kupanda mlima Kilimanjaro.