***********************
Na Muhidin Amri,
Tunduru
MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro, amewataka madiwani wilayani humo kuwa mstari wa mbele katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotokana na fedha za Serikali.
Mtatiro aliyasema hayo jana mjini Tunduru, wakati akizungumza na Madiwani na baadhi ya Wakuu wa idara katika semina ya kuwawezesha madiwani uelewa wa majukumu yao,kuwajengea uwezo na kufahamu kanuni mbalimbali zinazoongoza mabaraza ya madiwani.
Alisema,ni muhimu kwa madiwani wakawa sehemu ya mipango ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita,hivyo wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kwa kusimamia na kutekeleza miradi katika Halmashauri yao.
“mkiona kuna kitu hakiendi sawa kwenye utekelezaji wa miradi mna wajibu wa kuchukua hatua kwa kutoa taarifa kwa viongozi wa juu ili lifanyiwe kazi,madiwani mna dhamana kubwa ya kufuatilia na kusimamia miradi katika Halmashauri yenu”alisema.
Aidha,amewataka kushirikiana na wananchi na watendaji kubuni na kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kuanzisha miradi ambayo itaongeza mapato,badala ya kusubiri fedha za ruzuku kutoka Serikali kuu.
Katika hatua nyingine Mtatiro ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo amewaomba madiwani kwenda kutoa elimu kuhusu umuhimu wa ulinzi na usalama kwa kuwafichua baadhi ya watu wanaowatilia shaka ambao hawafamiki vyema katika maeneo yao.
Alisema, kumekuwepo na taarifa ya kuwepo kwa watu wenye viashiria vya vitendo vya ugaidi katika mkoa jirani wa Mtwara na wilaya hiyo imepakana na mkoa huo kwa hiyo ni vyema na wao wakachukua tahadhari.
Naye Afisa Serikali za mitaa kutoka Ofisi ya Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Amandus Chilumba alisema, wameamua kufanya mafunzo kwa Halmashauri za mkoa huo kwa lengo la kuboresha utendaji kazi kwa watumishi mbalimbali ngazi ya Halmashauri wakiwemo madiwani.
Alisema, mafunzo hayo ni muhimu kwani yataongeza uelewa dhidi ya usimamizi wa fedha,manunuzi na utawala hasa wakati huu ambao Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia fedha za UVICO-19.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Masonya Said Bwanali,ameipongeza serikali kwa kutoa mafunzo hayo kwani yanakwenda kuwaongezea uelewa mkubwa juu ya usimamia wa fedha,kutambua majukumu yao na kujenga mahusiano kati ya madiwani na watumishi.
Bwanali mabye ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, ameiomba Serikali kutoa mafunzo kwa Halmashauri nyingine za mkoa wa Ruvuma na Nchi kwa jumla kwani yatasaidia sana kuongeza uelewa katika kubuni vyanzo vingi na kusimamia mapato yatakayopatikana.
Diwani wa kata ya Namakambale Mfaume Wadali alisema, mafunzo hayo yanakwenda kuongeza tija katika Halmashauri yao na watakuwa na watu wenye uelewa na uwezo wa kujenga hoja katika vikao mbalimbali vya mabaraza ya Madiwani.
Pia alisema, baada ya mafunzo watakwenda kufanya kazi kwa ushirikiano na kila upande kutambua majukumu yake, hivyo kuepusha malumbano yasiokuwa na faida kwa Halmashauri.