Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Innocent Bashungwa akipokea kombe la mshindi wa jumla wa tatu kwenye mashindano ya SHIMIWI kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Pauline Gekul akipokea kombe la mshindi wa pili wa mchezo wa karata kwenye mashindano ya SHIMIWI kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi
***************************
Na. John Mapepele, WUSM
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Innocent Bashungwa, (Mb), kesho, Novemba 22, 2021 atazindua mambo sita ya kimageuzi katika Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mambo hayo ni Uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, Mfumo wa Kidigitali wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bodi ya Filamu nchini, COSOTA, Mashindano ya Michezo ya Samia Taifa cup na kuwaunganisha wadau wa sekta hizo jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi matukio hayo sita ya kimkakati na kimapinduzi yanakwenda kutokea kesho wakati nchi yetu inaadhimisha mwaka miaka sitini ya uhuru wake.
Matukio haya ya kimkakati yatasaidia kuongeza ajira na kuinua vipato na vipaji vya wasanii na wachezaji hivyo amewataka wasanii na wachezaji kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia taaluma zao ili kuiingiza Tanzania kwenye ngazi za kimataifa na kuinua uchumi wa nchi yetu.
“Kufufuliwa kwa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa na uzinduzi wa Bodi utakaofanywa kesho utawawezesha wasanii kupata mikopo ya masharti nafuu hivyo kupata wazalishaji, watengenezaji, na wawekezaji wakubwa, wa kati na wadogo katika tasnia hii hapa nchini” amefafanua Dkt. Abbasi
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa nchini. Dkt.Emmanuel Ishengoma amesema kwa upande wa mifumo, kila mfumo wa kidigitali katika kila taasisi (BASATA, Bodi ya Filamu na COSOTA) utasaidia wasanii na waombaji wengine wa huduma kwenye taasisi hizo ikiwemo vibali vya matamasha na vibali vya safari za nje kutoka popote walipo duniani kupata bila kwenda katika ofisi za taasisi hizo kama ilivyokuwa hapo awali, hivyo kurahisisha upatikanaji wa huduma, kupunguza muda na gharama.
Aidha, mfumo wa Kidigitali wa BASATA utasaidia kusajili wasanii na kutoa vibali vya kuendesha shughuli za Sanaa ambapo Mfumo wa Bodi ya Filamu utafanya kazi ya kusajili, kuhakiki filamu na kutoa vibali vya kuendesha shughuli za filamu, wakati Mfumo wa HAKIMILIKI ambao pia umetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa utafanya kazi ya kusajili wanachama wa COSOTA, kusajili kazi zao na kutoa leseni za matumizi ya kazi za ubunifu.
Akizungumzia kuhusu mashindano ya Samia Taifa Cup Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Omary Singo amesema mashindano hayo yataaanzia katika ngazi ya kila mikoa ili kupata timu bora na fainali zake zitafanyika jijini Dar es Salaam, Disemba 10 – 16, 2021 kwenye viwanja vya Benjamin Mkapa, Uhuru na Uwanja wa Ndani wa Taifa na kwa kuanzia yatashirikisha michezo mitatu ambayo ni Soka kwa wanaume na wanawake, Netiboli kwa wanawake na Riadha kwa wanaume na wanawake
Singo ametoa wito kwa wadau wa michezo kuja kushuhudia michezo hiyo ambapo amesema mashindano hayo yatahusisha pia mashindano ya fani anuai za Sanaa hivyo kuleta hamasa na vionjo vya namna yake.