Waziri wa Wizara hiyo,Balozi Liberata Mulamula,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo November 20,2021 jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Wizara ya Mambo ya Nje,Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
WIZARA ya Mambo ya Nje,Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema Tanzania inajivunia mchango wake katika juhudi za kuhakikisha uwepo wa amani, ulinzi na usalama Barani Afrika na duniani kwa ujumla, katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru Tanganyika.
Hayo yameelezwa leo Novemba 20,2021 Jijini Dodoma na Waziri wa Wizara hiyo,Balozi Liberata Mulamula wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Wizara ya Mambo ya Nje,Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kipindi cha miaka 60, ya uhuru wa Tanganyika.
Waziri Mulamula amesema Tanzania inajivunia mchango wake katika juhudi za kuhakikisha uwepo wa amani, ulinzi na usalama Barani Afrika na duniani kwa ujumla, katika kipindi cha miaka 60 iliyopita.
“Katika kipindi hicho, Tanzania imeshiriki katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo kwenye nchi mbalimbali duniani. Ushiriki wa Tanzania katika harakati hizo umekuwa wa moja kwa moja au kupitia jumuiya za kikanda.
“Kwa mfano, mwaka 1999 Tanzania ilishiriki katika kuzipatanisha pande mbili zilizokuwa zikihasimiana nchini Burundi. Mpatanishi Mkuu katika mgogoro huo alikuwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kabla ya kifo chake na baadaye juhudi hizo ziliendelezwa na Hayati Benjamini Mkapa, Rais wa Awamu ya Tatu.
“Usuluhishi wa mgogoro huo ulitamatishwa kwa pande zinazohasimiana kusaini Makubaliano ya Amani na Maridhiano ya Arusha mwaka 2000 na Makubaliano ya Kusitisha Mapigano mwaka 2005, ambayo yamedumisha amani nchini Burundi hadi hivi sasa.
“Mwaka 2015 Jumuiya ya Afrika Mashariki ilimteua Hayati Benjamin Mkapa kuongoza Majadiliano ya Amani ya Burundi baina ya pande zilizokuwa zikihasimiana nchini humo kufuatia mgogoro wa kikatiba uliombatana na machafuko yaliyotokana na tofauti za kisiasa,”amesema.
MAFANIKIO YA KIUCHUMI
Pia amesema Tanzania imepata mafanikio ya kiuchumi kupitia uhusiano baina yake na nchi nyingine, jumuiya za kikanda na mashirika ya kimataifa.
“Uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na nchi nyingine unatokana na uwepo wa mikataba na makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Mathalan, kupitia makubaliano ya ushirikiano katika biashara baina ya Tanzania na nchi za Oman, Qatar, Kuwait na Saudi Arabia, nchi yetu inauza mbogamboga, nyama na bidhaa za nyama katika masoko ya nchi hizo.
Kadhalika, kupitia makubaliano ya hivi karibuni ya biashara kati ya Tanzania na China, kampuni 72 za kitanzania zimepata ithibati kutoka katika mamlaka za China kuuza maharage ya soya katika soko la nchi hiyo ambapo zaidi ya tani 120 za bidhaa hiyo tayari zimeuzwa nchini humo,”amesema.
AWATAKA WATANZANIA KUCHANGAMKIA FURSA YA KISWAHILI NJE YA NCHI
Katika hatua nyingine,Waziri Mulamula amewataka watanzania kuchangamkia fursa ya kufundisha lugha ya Kiswahili nje ya Nchi ambapo amedai soko na mahitaji ni makubwa.
“Rai yangu watanzania tuchangamkie fursa tusingoje vya kupewa Nchi jirani wanachangamkia sana,Sasa hivi tupo katika mkakati tunapeleka watu wanaofaa na wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo na mahitaji ni mengi wana Diaspora wanatusaidia,”amesema.