Naibu Katibu Mkuu wa EAC ,Mhandisi Stephen Mlote akizungumza katika kongamano hilo jijini Arusha.
Mbunge wa bunge la EAC kutoka Tanzania,Injinia Pamela Maasay akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano huo.
Mkurugenzi wa shirika la MIMUTIE ,Rose Njilo akizungumza kuhusiana na nafasi ya mwanamke kushiriki uongozi katika mkutano huo.
Mkurugenzi wa shirika la SASA Foundation lililopo mjini Arusha,Jovita Mlay akizungumza katika kongamano hilo
………………………………………………………………………………
Happy Lazaro, Arusha.
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ,Mhandisi Stephen Mlote amewataka wanawake katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na barani Afrika kwa ujumla kuwa mstari wa mbele na udhubutu katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi .
Ameyasema hayo jijini Arusha wakati akizindua kongamano la wanawake lililoandaliwa na Mtandao wa wanawake wa maendeleo na mawasiliano barani (FEMNET)lenye lengo la kuimarisha ushiriki wa wanawake katika masuala ya kisiasa barani Afrika,ambapo amesema wanawake wanayo nafasi kubwa ya kugombea nafasi hizo kwani hata katika bunge la EAC zipo nafasi maalumu kwa ajili ya wabunge wanawake.
Amesema kuwa,wanataka kuhamisha wanawake kugombea nafasi mbalimbali ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwani hapo awali kulikuwa na hofu kuwa nafasi hizo ni kwa ajili ya wanaume tu,hivyo kuwataka kuchangamkia fursa hiyo ambayo inahitaji nafasi mbalimbali za uongozi.
Mhandisi Mlote amesema jumuiya ya Afrika mashariki wanahakikisha katika masuala ya uongozi kunakuwa na usawa kwani nyumba bila mwanamke itakuwa haina maendeleo hivyo wajiamini na kufikia uongozi katika ngazi za kimataifa.
Mbunge wa Bunge la jumuiya ya Afrika Mashariki Mhandisi Pamela Maasay ambaye pia ni msemaji wa wanawake wabunge wa jumuiya hiyo amesema kuwa, sababu kubwa za wanawake kutokushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi ni kutokana na misingi ambayo iliyojengwa tayari kwenye jamii jambo linalowafanya baadhi ya wanawake kuwa waoga.
Mhandisi Pamela ameongeza kuwa ,uoga wa kwanza unatokana na athari za mfumo dume uliokuwepo awali hasa kwenye kufikiria kuingia kwenye kuwania nafasi za uongozi na hasa za kisiasa kwasababu wameaminishwa na katika jamii inaoneshwa kwamba wanawake ni watu ambao hawawezi.
Amesema kuwa, sababu nyingine ni kwamba siasa za Afrika zinahitaji rasilimali fedha na asilimia kubwa ya wanawake ambao wapo kwenye nchi za Afrika bado ni wanawake ambao wapo kwenye vipato vya chini, ni wajasiriamali ambao wakifikiria kujiingiza kwenye siasa waaminu ya kwamba hawatakuwa na vipato vya kutosha kuweza kujitosheleza kufanya kampeni na mahitaji mengine.
Mhandisi Pamela akingumzia kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki kuwa na Rais mwanamke ambaye ni Rais wa Tanzania Mh Samia Hassan Suluhu ambapo amesema kuwa, ni chachu kubwa kwa wanawake wadogo yaani mabinti kwa sababu katika historia hasa Tanzania hawajawahi kuona mwanamke kiongozi hasa kwa nafasi ya juu kama Rais.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika la MIMUTIE ,Rose Njilo ambaye ni mmoja wa wagombea wa ubunge katika la jimbo lilioachwa wazi na marehemu William ole Nasha amesema kuwa ,wanataka kuifahamisha Dunia kuwa wanawake wanaweza kuwa viongozi ambapo yeye ni mwanamke wa jamii ya kifugaji lakini hakusita wala kuogopa kugombea kati ya wanaume 17 pamoja na kuwa bado katika jamii za kifugaji kuna dhana kuwa mwanamke hawezi kuongoza.
Amesema kuwa, wakati anashiriki katika kinyang’anyiro hicho jamii ilimuona kama mtu ambaye amekiuka Mila na desturi kwa sababu bado mfumo dume umeshika hatamu kwa jamii hiyo kwani bado wana changamoto kubwa, kazi na safari ya kuelimisha jamii hususan akina baba kwani wanawake angalau kwa sasa wamepata mwamko.
“Nakumbuka wakati nasimama kusema sera zangu walikuwa wanasema kuwa nafaa ila tatizo ni sababu mimi ni mwanamke kwa hiyo bado Mila na desturi zetu hazitutambui sisi wanawake kuwa tunaweza kuwa viongizi bora, Alisema Rose Njilo.
Naye Mkurugenzi wa shirika la SASA Foundation ,Jovita Mlay amesema kuwa ,bado mwamko wa wanawake kugombea nafasi ni mdogo kutokana na hofu ya kujiona kuwa hawawezi,hivyo amewataka kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali ili kuwepo na uwiano sawa katika uongozi Kati ya wanaume na wanawake.