Hayo yamesemwa na mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela wakati akifungua kongamano la kimataifa wa uwazi, uwajibikaji na utawala bora (ITAC) kwa niaba ya waziri wa fedha na mipango Dkt Mwigulu Nchemba.
Mongela amesema kuwa, utawala bora, uwazi na uwajibikaji kwenye mifumo na sekta zote unaanzia kwenye bajeti, usimamizi wa matumizi, mapato ya serikali lakini pia kuwa wawazi kwamba wadau wote wawe na uwezo wa kupata taarifa bila urasimu.
“Kwa niaba serikali mheshimiwa makamu wa Rais amedhirisha kuwa siku zote serikali yetu inazingatia misingi ya utawala bora kwani imeunga mkono juhudi hizi za wadau za kuhakikisha kwamba vigezo vya uwazi na uwajibikaji vinazingatiwa,”amesema Mongela.
Amesema kuwa, kwa dhana moja watahakikisha kwamba rasilimali za taifa ambazo viongozi wamepewa dhamana ya kusimamia kwa niaba ya wananchi zinasimamiwa vizuri na wananchi wanaona waziwazi faida ya dhamana hiyo na maendeleo ya nchi kuwagusa moja kwa moja.
Kwa upande wake CPA Ludovick Utoh Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali mstaafu ambaye ni Mkurugenzi wa tasisi ya WAJIBU amesema kuwa, madhumuni ya kongamano hilo la siku mbili inatokana na dhana ya uwazi na uwajibikaji katika kuleta makusanyo na matumizi bora zaidi ya fedha za umma kwaajili ya kuletea watu maendeleo
“Taasisi ya WAJIBU tunafarijika sana tunapoona kinachofanyika kwani miezi miwili mitatu Rais wetu Mh Samia Hassan Suluhu aliwajulisha watanzania kwamba serika imekopa fedha na akaeleza kwa undani matumizi ya zile pesa na huo ndio uwazi tunataka kuuona katika utendaji kazi wa serikali,” amesema CPA Utoh.
Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo Magreth Gudluck Msemo amesema kuwa kutokana na majadiliano na ripoti iliyozinduliwa wameweza kujua ni kwanini wananchi wanapaswa kujua nini kinachofanyika katika nchi lakini pia kujua namna gani fedha zinatumika pamoja na kujua haki zao kama mwananchi na wajibu wa kuuliza jambo.