………………………………………………………
Na Silvia Mchuruza,BUKOBA
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera mh Murshid Ngeze amemuomba mkurugenzi wa halmashauri hiyo kufuatilia mienendo ya ukusanyaji wa mapato katika kila kata ili kusaidia halmashauri kujua maendeleo ya miradi katika kata hizo kwa urahisi.
Ngeze ametoa kauli hiyo katika kikao cha baraza la madiwani cha robo ya mwaka kilichofanyika katika ukumbi wa halimashauri hiyo uliopo eneo la chemba manispaa ya Bukoba.
Amesema kuwa kunatakiwa kuwepo kwa taarifa ya kila kata ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato ili kuleta usimamizi mzuri wa mapato katika kila kata na kuweza kuongeza mapato ya halimashauri hiyo.
“Mkurugenzi we na timu yako sasa nikuombe kuna aja ya kukaa sasa na madiwani wetu kujua kipi kimepatikana na changamoto yao ni ipi na wamekwama wapi na usimamimizi wa mapato katika kata uende vizuri ili tuweze kutambua ni nini kinakwamisha mapato hayo”. Alisema Ngeze.
Aidha mwenyekiti huyo amesema kuwa taarifa hizo zitasaidia kujua miradi ya maendeleo imefikia kiwango gani cha ujenzi na kujua changamoto inayoikabili miradi hiyo ili kuweza klutatuliwa.
Kauli hiyo imekuja kufuatia uwepo wa kituo cha mafuta katika kata ya Kyaitoke Halmashauri ya wilaya ya Bukoba ambacho hakilipi ushuru kwa Halmashauri hiyo na hivyo kuikosesha halimashauri mapato.