Katibu wa Kikundi cha Wabunge Vinara wa Usalama wa
Chakula, Mhe Salome Makamba kushoto akiwa na wabunge vinara wa usalama na chakula wakati mkutano wa Siku mbili wa Wadau wa
Lishe
Chakula, Mhe Salome Makamba kushoto akiwa na wabunge vinara wa usalama na chakula wakati mkutano wa Siku mbili wa Wadau wa
Lishe
**************************
NA OSCAR ASSENGA,TANGA
Wabunge Vinara wa Usalama wa Chakula wamesema kwamba watapelekea mapendelezo Bungeni ili kuiomba Serikali iweze kuongeza kiwango cha fedha ya lishe ya mtoto inayotengwa kila Halmashauri ya Sh.1000 kiweze kubadilishwa badala yake wapewe kwa asilimia.
Hayo yalisemwa leo na Katibu wa Kikundi cha Wabunge Vinara wa Usalama wa Chakula, Mhe Salome Makamba ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa Kikundi hicho Mhe Neema Lugangira katika Mkutano wa Siku mbili wa Wadau wa Lishe.
Mkutano huo wenye kaulimbiu “Lishe Bora ni Msingi wa Maendeleo ya Mtaji wa Binadamu katika Uchumi wa Kishindani” uliowakutanisha wadau wa chakula na lishe uliofanyika jijini Tanga.
Mhe Salome Makamba, alisema sambamba na hilo wanaomba Serikali sikivu chini ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan iweze kuangalia upya suala la kupelekea masuala ya chakula kusimamiwa na TBS badala yake isimamiwe na chombo maalumu tofauti kwa sababu TBS haiwezi kuthibitisha ubora na wakati huo huo kusimamia usalama
Katibu huyo aliiomba pia Serikali na wadau wote wakiwemo Watanzania waweze kusimamia suala la usafi na usalama wa chakula kwa sababu Tanzania ni nchi Tajiri na ina rasilimali nyingi.
“Tusimamie usalama wa chakula kutoka Shambani mpaka kwa mlaji na tuache kutupa chakula chini lakini Halmashauri zijenge vizimba ili chakula kiwepo mahali pa usalama na serikali iweze kusimamia kwenye masoko itasaidia kuweza kuwa na chakula salama na safi na kutengeneza Taifa bora” Alisema
Aidha alisema kwamba wanaipongeza Serikali kwa juhudi za kutengenza Sera, Kanuni na Sheria mbalimbali pamoja na changamoto zote na zipo changamoto ndogo ambazo wanaomba wafikishe ili waweze kusonga mbele kama Taifa kwa kuweka chakula salama kwenye nchi yetu na lishe bora.
Alisema wanaiomba Ofisi ya Waziri Mkuu iweze kukamilisha Sera ya Taifa ya Chakula na Lishe ambayo ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kwa tarkibani miaka mitatu sasa ipo tu hapo Ofisini na inatakiwa kufanya Maboresho ya Sera hiyo maana imeshapitwa na wakati.
Alisema na ikibidi kabla ya hawajamaliza kipindi cha Bunge wapeleke Bungeni mapendekezo ili iweze kutungiwa Sheria kama Sheria ya Usalama wa Chakula huku akiipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuandaa Mpango wa Lishe kwenye Kilimo.
Hata hivyo aliiomba Ofisi ya Waziri Mkuu wasaidie Wizara nyengine za Kisekta ziweze kutengeneza Mpango wa Lishe wa kisekta kama ambavyo Wizara ya Kilimo imefanya