Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel ameanza ziara ya kikazi katika Mkoa wa Kagera na kupokelewa na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa huo Meja Jenerali Charles Mbuge.
Akiwa mkoani Kagera Dkt. Mollel leo atashiriki katika uzinduzi wa Mpango wa Kikanda wa Mapambano dhdi ya Ugonjwa wa Malaria katika Nchi za Maziwa Makuu unaohusisha nchi za Tanzania, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Demokrosia ya Congo, Uganda, Kenya pamoja na Sudani ya Kusini.
Uzinduzi huo kwa nchi ya Tanzania na Rwanda unatarajiwa kufanyika Wilayani Ngara katika Mpaka wa Rusumo unaotenganisha Tanzania na Rwanda.
Katika mazungumzo yao, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge amesema kuwa Mkoa huo uko juu katika maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwa 15.4% huku kiwango maambukizi ya ugonjwa huo kitaifa ni 7.4% na kusema kuwa Ugonjwa Malaria bado ni tishio katika Mkoa huo.
Aidha Meja Jenerali C. Mbuge amesema kuwa Mkoa huo umepokea fedha kiasi cha Tsh Bilioni 20 kutoka katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo na mapambano dhidi ya UVIKO-19 fedha ambazo zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kumshurku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
Kuhusu hali ya utoaji wa Chanjo ya UVIKO-19, Meja Jenerali C. Mbuge amesema kuwa Mkoa huo awali ulipokea dozi 45,000 ambazo zote zilikwisha na kuongezewa tena dozi zaidi ya 61,000.
Dkt. Mollel amewataka wataalam wa afya pamoja na Taasisi za Afya mkoani Kagera kutoa ushirikiano kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na watendaji wengine wa Serikali.
Amewataka watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa wananchi pamoja na kuendelea kutoa elimu ya UVIKO-19 na kuhamasisha wananchi kupata chanjo.
Kuhusu miradi inayoendelea na ile itakayotekelezwa kupitia fedha zilizotelewa kupitia Mpango wa Maendeleo ya Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 Dkt. Mollel amewataka watendaji kusimamia vyema miradi hiyo na kuitekeleza ndani ya wakati huku akiwaonya wote ambao watahusika katika rushwa na hujuma za miradi hiyo kuchukuliwa hatua kali za kisheria.