- Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeingia makubaliano na Benki ya KCB ili kuwawezesha Wachimbaji Wadogo kupata mikopo endelevu na kwa urahisi zaidi ili waweze kufanya shughuli za uchimbaji madini zenye tija.
- Makubaliano yamefikiwa leo
Novemba 16, 2021 baada ya kusaini Hati ya Makubaliano (MOU) baina ya pande hizi mbili katika ofisi za STAMICO jijini Dar es Salaam. - Akiongea wakati wa hafla ya utiaji saini Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema STAMICO imeamua kubeba jukumu la kuwa kiungamnishi kati ya wachimbaji wadogo na Benki ya KCB ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kukua na kuwa wachimbaji wa kati na wakubwa.
- Amesema Katika makubaliano hayo STAMICO itawajibika kutoa utaalam elekezi katika maeneo ya Jiolojia, Uchimbaji na Uchenjuaji Madini kwa miradi ya Wachimbaji Wadogo ambayo itafanya maombi ya mikopo na kuiwasilisha kwa Benki kabla ya utekelezaji wake.
- Dkt. Mwasse ameongeza, kuwa wachimbaji wadogo wana umuhimu na faida kubwa katika kukuza uchumi wa nchi, hivyo makubaliano haya ya uwezeshaji yatawasaidia kuweza kuchimba kwa tija na kuweza kuchangia katika pato la Taifa na kuongeza ajira kwa Watanzania.
- Amewataka wachimbaji wadogo kufuata taratibu zilizowekwa na kuheshimu makubaliano ili kuweza kunufaika na mpango huu wa kuwezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo kutoka taasisi za fedha ambazo zimeonesha nia ya kuwasaidia.
- Kwa upande wa Benki ya KCB, mkuu wa kitengo cha huduma za Kiislamu (Islamic Banking) Bw. Amour Muro amesema, Benki ya KCB imeitika wito wa Serikali wa kuwasaidia wachimbaji wadogo kifedha ili kuimarisha shughuli zao za uchimbaji na imeamua kukaa karibu na wachimbaji hao ili kuweza kutatua changamoto zao.
- Amesema katika ,makubaliano hayo Benki ya KCB itawajibika kutoa mikopo kwa Wachimbaji Wadogo ambao watawasilisha maombi ya mikopo katika maeneo ya miradi ya uchimbaji madini itakayokidhi vigezo.
- Muro amesema KCB imeamua kushirikiana na STAMICO ili kuweza kupata ujuzi wa kitaalamu kuhusiana na uchimbaji mdogo kwa kuwa Shirika hili lina uzoefu wa kutoshakatika sekta ya uchimbaji wadogo hivyo anaamini ushirikiano huu utawawezesha kuweka taratibu zitakazowawezesha kutoa mikopo kitaalamu.
-
Amesema KCB tayari imeshatumia kiasi cha zaidi ya shilingi Bilion 4.5 kutoa mikopo katika Sekta ya uchimbaji madini na sasa imeamua kujipambanua katika sekta ya uchimbaji mdogo ili kuleta tija na kuwafikia wachimbaji wengi zaidi.
STAMICO ikiwa ndiyo Mlezi wa Wachimbaji Wadogo inaendelea kutekeleza mikakati yake ya kuendeleza shughuli za uchimbaji mdogo nchini ili uwe wenye tija na kuchangia ipasavyo katika uchumi wa nchi yetu.