…………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema watendaji ambao wataonekana kuwa ni sehemu ya migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa kero kubwa kwenye mkoa huo ,watawajibishwa.
Kunenge aliyasema hayo mjini Kibaha wakati wa mkutano wa mashauriano kuhusu Mpango wa kukabiliana na migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wa wengine wa ardhi kwa kutumia mfumo wa ranchi ndogo kwenye mkoa huo.
Amesema ifike wakati migogoro hiyo iishe na ibaki historia na mkoa hauwezi kuwafumbia macho watendaji na wataalamu ambao wataonekana kuwa wanashiriki kwenye migogoro hiyo ambayo imesababisha viongozi kutofanya shughuli nyingine na kubaki kusuluhisha migogoro hiyo.
“Tumechoshwa na migogoro hii wakati viongozi wapo njia ziko mbili tu ni kutatua au kuachia ngazi maana inaonekana kazi zimewashinda kwani hali hiyo inasababisha wakati mwingine watu kupotea maisha,” alisema Kunenge.
Naye mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainab Abdala amesema kuwa migogoro hiyo ni kero kubwa sana ambapo wakati wanaitatu wanapigiwa simu na baadhi ya vigogo.
Abdala amesema kuwa wafugaji hao wamekuwa wakitumika na baadhi ya watu wenye uwezo ambao ndiyo wanaowakingia kifua na kusababisha wafugaji kukosa haki zao.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa changamoto kubwa ni wafugaji wavamizi kuingia kwenye maeneo ya wafugaji bila ya kufuata sheria.
Ridhiwani amesema utaratibu wa wafugaji kuingia upo lakini haufuatwi ambapo wafugaji wenyeji ambao walitengewa maeneo yao hawana vurugu kwani wanaishi kwa utaratibu.