………………………………………………..
NA Zillipa Joseph,Katavi
Mkoa wa Katavi umefanikiwa kuzuia vifo vya watoto njiti kufuatia kuwepo kwa uangalizi wa karibu ikiwemo kinamama kufundishwa njia ya kangaroo kulea watoto; pamoja na kuwepo kwa vifaa maalum vya kusaidia watoto kupumua kwa ajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya kutimiza muda wao.
Bwana Daudi Bahuta ni Muuguzi wa wadi ya wazazi kitengo cha watoto njiti katika hospitali ya Teule ya Rufaa ya mkoa wa Katavi alisema kwa wiki wanazaliwa watoto kati ya watatu hadi kumi na tano.
Alieleza kuwa watoto njiti wanaozaliwa katika zahanati pia wanafikishwa hospitalini hapo kwa uangalizi zaidi.
“Hapa tuna chumba hiki maalum ambacho tunawaweka watoto waliozaliwa kabla ya muda wao kutimia lakini pia na wale watoto ambao hawana uzito wa kutosha” alisema Bahuta.
Ameongeza kuwa kinamama wanaojifungua watoto njiti wanafundishwa kulea watoto kwa njia ya kangaroo lakini pia zipo mashine za kusaidia kupumua ambazo wanatumia watoto wanaoshindwa kupumua vizuri.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto ambaye pia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali Teule ya Rufaa ya mkoa wa Katavi Dk. Yustina Tizeba amesema sababu zinazochangia kuzaliwa kwa watoto hao ni pamoja mama mjazito kuugua magonjwa mbalimbali.
Dk. Tizeba aliyataja magonjwa hayo kuwa ni pamoja na malaria, U.T.I, shinikizo la damu, nk.
Aidha amewashauri kinamama wajawazito kufika kliniki mapema mara tu wanapogundua kuwa ni wajawazito kwa ajili ya kupata ushauri.
Kwa upande wao kinamama waliojifungua watoto njiti wamesema wamepata elimu ya kutosha namna ya kulea watoto wao.
Yusta Masonga ni mkazi wa Kigamboni katika Manispaa ya Mpanda yeye amejifungua watoto njiti mapacha, amesema watoto wake walizaliwa wakiwa na uzito mdogo na amekaa hospitalini hapo kwa wiki mbili sasa.
“Namshukuru Mungu kwa kunipatia mapacha, na hivi leo nimeruhusiwa kutoka nitakwenda kufuata ushauri wa daktari na ninaamini watoto wangu watakua” alisema Yusta.