………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
MBUNGE Wa Bagamoyo Muharami Mkenge Pamoja na madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo, wameshtushwa na hoja ya upotevu wa dawa katika hospital na vituo vya afya hali iliyosababisha Halmashauri hiyo kuingia kumi bora kati ya Halmashauri zinazoongoza kwa upotevu wa dawa nchini ,mwaka 2020/2021.
Rekodi hiyo imetajwa kuwepo katika ripoti ya wizara ya afya, ambapo Mkenge amesema ni aibu na lazima hatua zichukuliwe ili kupambana na upotevu huo.
Akitoa dukuduku lake wakati wa kikao cha madiwani Halmashauri ya Bagamoyo, alisema wizi wa dawa mbalimbali unasababisha wananchi kukosa dawa wakati mwingine hata Panadol kwenye hospital na vituo vya afya na badala yake kupata shida kwenda katika maduka ya nje.
“Mara kadhaa tumekuwa tukipokea malalamiko kwa wananchi kuhusu kukosa dawa hospitalini ,kumbe wapo baadhi ya watumishi wa afya wanadokoa madawa haya kwa maslahi yao ama vinginevyo,hatuwezi kukaa kimya,nimepokea taarifa ya wizara Kama Mbunge mwakilishi wa wananchi imenisikitisha sana ,
“Tunatia aibu kwani hali hii sio nzuri na ripoti hii haifurahishi, alifafanua Mkenge.
Wakijadili juu ya hoja hiyo, baadhi ya madiwani akiwemo diwani wa kata ya Magomeni Mwanaharusi Jarufu alisema, wazee,watoto wamekuwa wakipata shida ya ukosefu wa baadhi ya dawa hili halikubariki.
“Kama madiwani Lazima tuseme jambo ili kukomesha wizi huu,ili tuwaondolee kero ya kukosa dawa kwa wananchi:”alisisitiza Jarufu.
Pia alizungumzia kero ya dampo la Sanzale kujaa pasipo kusukumwa Wala kutiwa dawa takriban mwaka na miezi miwili Sasa hali inayotishia magonjwa ya mlipuko.
Jarufu aliomba fedha itengwe ili kusukuma dampo hilo kwani ni vipindi vinne mfululizo hakuna matokeo.
Nae diwani kata ya Dunda, Hafsa Kilingo alieleza, hoja ya mkaguzi imeshapita, hivyo iangaliwe namna ya kukabiliana na tatizo hilo kwa maslahi ya Umma.
Alisema haiwezekani wakawa wanahimiza wananchi kujiunga na Bima halafu wakifika hospital wanakosa huduma.
Diwani wa Kisutu Muhidin Aweso alibainisha kwamba, Serikali imekuwa ikihangaika kuongeza bajeti ya dawa kusaidia wanyonge na wananchi wake ikitokea mtumishi wa afya anabainika kwenda kinyume na juhudi hizo inabidi hatua za kinidhamu zichukuliwe.
Aweso alisema ,madawa hakuna katika hospital na vituo vya afya kumbe inasababishwa na wizi na upotevu usioeleweka ,kiukweli inaumiza.
Mganga mkuu wa wilaya ya Bagamoyo dokta Lugano Mwakipesile alisema yeye hana taarifa hiyo, ndio kwanza ameisikia na kudai ni ripoti ya mwaka wa fedha uliopita.
Pamoja na hilo ,alisema amepokea maelekezo yaliyotolewa na kuahidi kuyafanyia kazi ambapo pia ipo mikakati waliyojiwekea ikiwemo kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya juu ya miongozo ya utunzaji wa dawa ili kuondoa tatizo la upotevu wa dawa.
Dokta Mwakipesile alieleza, baada ya mafunzo hayo yeyote atakaebainika kusababisha upotevu wa dawa atachukuliwa hatua.