*******************************
Na Lucas Raphael, Ngara
SERIKALI imetoa kiasi cha sh bil 2.7 kwa halmashauri ya wilaya ya Ngara Mkoani Kagera kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika shule za msingi na sekondari ikiwemo hospitali ya wilaya na zahanati ya mumuhamba.
Akiongea na Mwandishi wa gazeti hili jana Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Solomon Kimilike alisema fedha hizo zimetolewa ikiwa ni sehemu ya Utekelezaji Mpango wa Maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Alisema kati ya fedha hizo sh bil 1.54 zimeelekezwa kwenye ujenzi wa vyumba 77vya madarasa na samani zake katika shule 23 za sekondari kwa ajili ya wanafunzi wapya wa kidao cha kwanza, utekelezaji kazi hiyo umeanza.
Aliongeza kuwa fedha hizo kiasi cha sh mil 780 zimeelekezwa kwenye vituo vya shule shikizi 6 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 39 vya madarasa na samani zake vinavyotoa huduma ya awali kwa watoto.
Aidha Kimilike alibainisha kuwa fedha kiasi cha sh mil 300 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa jengo la dharura katika hospitali ya wilaya hiyo ya Nyamiyaga na sh mil 90 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya watumishi 2 katika zahanati ya Mumuhamba.
Alieleza kuwa katika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati na kwa gharama nafuu, watatumia mfumo wa fosi akaunti (force account) ambapo manunuzi ya vifaa vyote yatafanywa na halmashauri.
Mkurugenzi alibainisha mikakati mingine iliyofanyika ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati kuwa ni pamoja na kufanya manunuzi ya pamoja ya vifaa vyote kutoka viwandani au kwa wauzaji wa jumla.
Mikakati mingine ni Wakuu wa idara kupangiwa Kanda za Usimamizi, kuunda Kamati za usimamizi katika ngazi za shule na vifaa visivyo vya viwandani mfano tofali za kuchoma, mawe, mchanga, kokoto na mbao kununuliwa ndani ya wilaya.