****************************
Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
16,Nov
VIONGOZI wa umma wametakiwa kuwasilisha matamko ya Mali zao ambapo mwisho wa kuwasilisha taarifa hizo ni Desemba 31 mwaka 2021 .
Zoezi hilo linaelekea ukingoni hivyo atakaeshindwa kuwasilisha taarifa zake atakuwa amekiuka Sheria ya maadili ambapo hatua za kinidhamu zitachukuliwa ikiwemo kulipia faini ya sh.milioni moja ,ama kifungo cha mwaka mmoja jela.
Akielezea kuhusiana na Sheria ya maadili kwa madiwani wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ofisa wa maadili kutoka sekretariet ya maadili ya viongozi wa Umma Kanda maalum,Hamad Bakari Hamad alisema ,dirisha la uwasilishaji wa matamko hayo lilishafunguliwa tangu octoba mwaka uliopita na mwisho wa kupokea taarifa hizo ni mwishoni mwa mwaka huu.
Alisema , viongozi hao wanajua taratibu hizo ,yanapatikana katika sekretariet ya maadili ya viongozi wa Umma ama katika website ,kwa kupakua taarifa ,unajaza kisha wanatakiwa kuthibitisha kwa mwanasheria wa Serikali au wakili yeyote anayetoka mahakama ya Tanzania.
Hamad alitoa wito kwa viongozi hao wafuate maadili ya utumishi ili kutumikia wananchi kwa maslahi mapana ya Umma.
“Tupo chini ya ofisi ya Rais, hatupaswi kusema hatua tunazozichukua ,hatupitishi taarifa sehemu nyingine Kwani tunafanya kazi moja kwa moja na ofisi ya Rais ,Lakini haimaanishi kwamba hatufanyi kazi “alifafanua Hamad.
Nae diwani wa kata ya Yombo Muhammed Usinga alisema wamepokea taarifa na wanashukuru kupata elimu hiyo na kukumbushwa wajibu wao.
Alielezea kwamba,wapo tayari na yeye Ni miongoni mwa watakaokwenda kuwasilisha sehemu ya mali zake na namna alivyozipata.
Diwani huyo ,Usinga alisema hiyo Ni Sheria ,ambayo imetungwa na wawakilishi wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,hivyo Wana kila sababu ya kuisimamia na kutekeleza ili kujiepusha na adhabu .
Mwisho