Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania imefanya kikao chake tarehe 15 Novemba 2021, na kuridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha kwa kipindi cha mwezi Septemba na Oktoba 2021, ambao uliwezesha kuendelea kuwepo ukwasi wa kutosha katika sekta ya benki. Hali hii pia ilichangia mwenendo wa riba katika soko la fedha kuendelea kuwa tulivu na katika viwango vya chini. Aidha, ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi umeimarika kufikia asilimia 4.6 kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba 2021, kutoka asilimia 3.2 kwa mwezi uliotangulia. Kamati pia, imejiridhisha kuwa, kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi inatarajiwa kuendelea kuimarika kutokana na kuimarika kwa uchumi wa dunia, pamoja na hatua za kisera zilizochukuliwa na Benki Kuu ili kuchochea upatikanaji wa mikopo kwa riba nafuu. Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha na kufikia dola za Marekani bilioni 6.7 kwa mwezi Oktoba 2021, kiasi kinachotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban miezi 7, sanjari na lengo la nchi na makubaliano ya jumuiya za kikanda.
Kamati imebaini kuwa, kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia imekuwa chini kidogo ya matarajio ya awali kutokana na kuibuka upya kwa janga la UVIKO-19 katika baadhi ya nchi, na kupanda kwa bei za nishati duniani. Hata hivyo, ukuaji huu wa uchumi wa dunia unatarajia kuchangia kuendelea kuimarika kwa uchumi wa Tanzania. Kasi ya mfumuko wa bei duniani, imekuwa ikipanda, kutokana na kuongezeka kwa mahitaji na kupanda kwa bei za nishati duniani, hata hivyo, Benki Kuu nyingi duniani zinaona ongezeko hili kuwa ni la mpito, na hivyo kuendelea na sera ya fedha yenye kuongeza ukwasi. Kamati inaamini kwamba, kuongezeka kwa uzalishaji wa mafuta duniani kutapunguza kupanda kwa bei nishati, pamoja na hayo, kamati inasisitiza umuhimu wa kuendelea kwa upatikanaji wa chakula cha kutosha nchini, na uimara wa thamani ya shillingi dhidi ya fedha za kigeni kunakotarajia kupunguza athari ya kupanda kwa bei ya mafuta kwenye mfumuko wa bei.
Vilevile, Kamati ilijadili mwenendo wa hivi karibuni wa uchumi wa ndani na kuona kuwa ukuaji wa uchumi Tanzania Bara uliendelea kuimarika hadi kufikia asilimia 4.7 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2021. Mfumuko wa bei uliendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3-5, sanjari na makubaliano ya kikanda kwa nchi za EAC na SADC. Mfumuko wa bei unatarajiwa kusalia sambamba na lengo, licha ya kuongezeka kidogo tangu mwezi Juni 2021. Ukusanyaji wa mapato ulikuwa wa kuridhisha, huku mapato ya kodi yakiwa zaidi ya asilimia 90 ya lengo. Uchumi wa Zanzibar ulikuwa kwa asilimia 6.5 katika robo ya pili ya mwaka 2020 ikilinganishwa na ukuaji hasi wa asilimia 1.4 katika robo ya pili ya mwaka 2020. Mfumuko wa bei uliendelea kuwa chini ya lengo la asilimia 5, huku ukusanyaji wa mapato ukiwa sawa na asilimia 73.6 ya lengo. Sekta ya nje imeendelea kuimarika kutokana na athari za janga la UVIKO-19, ikiendelea kuwa na nakisi ndogo za urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji mali nchi za nje kutokana na kuanza kuingia kwa mapato yatokayo nje ya mauzo ya madini, mazao ya biashara na shughuli za utalii.
Kwa kuzingatia tathmini ya mwenendo wa uchumi wa hivi karibuni, pamoja na matarajio ya mfumuko wa bei kuendelea kubaki ndani ya lengo, Kamati ya Sera ya Fedha imeridhia Benki Kuu ya Tanzania kuendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi kwa kipindi cha mwezi Novemba na Desemba 2021 ili kuendelea kuimarisha uchumi.
Gavana
Benki Kuu ya Tanzania