Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Mhandisi Dkt. Samuel Gwamaka pamoja na watumishi wa NEMC Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wakiwa katika picha ya Pamoja na Prof. Mark Mwandosya walipofanya ziara Wilaya ya Kyela katika Safu ya Milima ya Livingstone.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Mhandisi Dkt. Samuel Gwamaka akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ikombe Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya kuhusu uchomaji moto katika Milima ya Livingston.
……………………………………………………………….
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na usimamizi wa Mazingira (NEMC) Mhandisi Dkt. Samuel Gwamaka afanya ziara katika safu ya milima ya livingstone Wilaya ya Kyela Kata ya Matema Mkoani Mbeya na kubaini Kuna uchomaji moto katika milima hiyo na kusababisha uchafuzi mkubwa wa Mazingira na uoto wa asili kupotea.
Dkt. Gwamaka akiwa katika Kijiji cha Ikombe eneo la lyulilo amezungumza na wananchi wa Kijiji hiko na kuwaeleza kuwa shughuli za uchomaji moto katika milima hiyo ni uharibifu wa Mazingira na unaathari kubwa kwa viumbe hai wanaoishi katika Hifadhi ya milima hiyo.
Aidha ameendelea kusema kuwa Milima ya Livingstone inagusa Mikoa mitatu ikiwemo Njombe ,Iringa na Mkoa wa Mbeya hivyo inapaswa kuwa na ushirikiano kati ya Mikoa hiyo ili kuweza kupambana na uharibifu wa Mazingira katika milima hiyo. Amesema kuwa Baraza linaendelea kutoa elimu kwa jamii ili wafahamu kuwa madhara ya uchomaji moto katika milima hiyo ni makubwa kwani itaathiri kizazi kilichopo na kijacho, kama tunavyoona hali iliopo sasa joto limeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na ukataji miti hovyo. Pia itambulike kuwa milima hiyo ndio kichocheo kikubwa cha upatikanaji wa maji katika mito yetu hivyo kunahaja ya kutunza na kuilinda
“Niwaombe wananchi wa Kijiji hiki na vingine kuhakikisha wanashirikiana na Serikali katika kusimamia hifadhi ya milima ya Livingstone ili kukilinda kizazi chetu na Taifa letu kwa ujumla. Kama tulivyo msikia Rais wetu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Hassan Suluhu akisisitiza Kila Wilaya kupanda miti million 1.3 na sio kupanda tu bali ni lazima miti hiyo itunze ili kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi. Hivyo mazingira ni yetu sote tuhakikishe tunashirikiana na mamlaka husika kama Wakala wa Misitu na Mamlaka ya Hifadhi ya wanyama pori ili kuendelea kuhakikisha maeneo ya Misitu na Hifadhi tunaendelea kulinda kwa Mustakabali wa Nchi yetu pamoja na vizazi vinavyokuja” Amesema Dkt. Gwamaka
Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Matema Bw. Charles Mwamamba amemshukuru Dkt. Gwaka kwa ujio wake kwani imeongeza nguvu kwa jamii na wananchi wa kijiji cha Ikombe na amesema kuwa matumaini yake elimu aliyotoa kwa wana kijiji hao itasaidia kuelewa kuwa wanapochoma moto wanasababisha madhara makubwa sana katika Mazingira. Ameendelea kusema kuwa historia ya Milima ya Livingstone ilikuwa na uoto wa kutosha lakini shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo, ukataji miti kwa ajili ya mkaa pamoja na uwindaji ndio zilizopelekea uharibifu huo kutokea.
Naye Meneja wa Kanda Nyanda za Juu Kusini NEMC Bi.Glory Kombe amesema kuwa milima ya Livingstone ni maeneo muhimu sana ambayo yanahitaji kuhifadhiwa hivyo sisi kama NEMC tutashirikiana na Halmashauri ya Njombe, Rudewa, Makete Rungwe na Kyela kuhakikisha tatizo hili la moto kutotokea tena kwa miaka ijayo na tutahakikisha milima hii inaifadhiwa ipasavyo. Pia tutahakikisha Sheria ya Mazingira inatekelezwa na kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika wanafanya uharibifu wa Mlima huu.