Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akihutubia wananchi baada ya kuzindua kiwanda cha kutengeneza na kusambaza bidhaa zitumikazo kwenye ujenzi wa majengo, miundombinu na viwanda vya utengenezaji magari cha (SIKA), kilichopo Salasala jijini Dar es salaam, Novemba 16, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia aina ya michanga inayofaa kutumika kwa ajili ya ujenzi, baada ya kuzindua kiwanda cha kutengeneza na kusambaza bidhaa zitumikazo kwenye ujenzi wa majengo, miundombinu na viwanda vya utengenezaji magari cha (SIKA), kilichopo Salasala jijini Dar es salaam, Novemba 16, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Meneja Uzalishaji kiwanda cha kutengeneza na kusambaza bidhaa zitumikazo kwenye ujenzi wa majengo, miundombinu na viwanda vya utengenezaji magari cha (SIKA), Mwijarubi Shida (kushoto), baada ya kuzindua kiwanda hicho kilichopo Salasala jijini Dar es salaam, Novemba 16, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua kiwanda cha kutengeneza na kusambaza bidhaa zitumikazo kwenye ujenzi wa majengo, miundombinu na viwanda vya utengenezaji magari cha (SIKA), kilichopo Salasala jijini Dar es salaam, Novemba 16, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
******************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda nchini kuwapokea na kuwapa ushirikiano watu wenye ulemavu ili waweze kupata fursa ya kuchangia katika shughuli za ujenzi wa Taifa kama Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini inavyotaka.
Ameyasema hayo leo (Jumanne Novemba 16, 2021) baada ya kuzindua kiwanda cha kampuni ya SIKA Tanzania kinachozalisha na kusambaza kemikali zinazotumika kwenye ujenzi wa miundombinu mbalimbali kilichopo Salasala. Pia Waziri Mkuu amefungua kinu namba mbili cha saruji katika kiwanda cha Twiga baada ya kukamilika kwa maboresho makubwa.
Akiwa kwenye viwanda hivyo kwa nyakati tofauti Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara na hivyo kuweza kuvutia wawekezaji wengi kutoka ndani na nje ya nchi.
“Wawekezaji njooni muwekeze Tanzania, tuna ardhi ya kutosha, umeme, barabara, tuna reli ya kati na tunajenga Reli ya Kisasa, pia tuna ndege 11 na nyingine zinakuja, tunajenga viwanja vya ndege kila mkoa, hivyo tunauhakika wa usafiri.”
Pia, ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara iendelee na utaratibu wa kukutana na Wizara au Taasisi za Serikali na Binafsi nchini ili kuwahamasisha kununua bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wafanyakazi wa viwanda hivyo kuwasaidia wawekezaji hao ili wakuze zaidi biashara zao na wanufaike na uwekezaji huo. “Kila mmoja asaidie ulinzi wa mali za kampuni, msikubali kushawishika kuhujumu viwanda hivi, vina manufaa kwetu.”
Naye, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo amesema ufunguzi na maboresho ya viwanda hivyo unaashiria kuboreshwa kwa mazingira ya biashara kati ya Tanzania na makampuni makubwa kama SIKA.
Kwa upande wake, Meneja Uzalishaji wa kiwanda cha SIKA, Mwijarubi Shida amesema kiwanda hicho kilianzishwa nchini mwaka 2015 na kilianza uzalishaji mwaka 2016. Amesema kiwanda kina jumla ya watumishi 37 kati ya hao 36 ni wazawa.
Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu kabla ya kuzindua kinu namba mbili katika Kiwanda cha Saruji cha Twiga, Mhandisi Hellen Simime alisema maboresho hayo yamechangia kuongeza jumla ya tani 140 katika uzalishaji wa saruji kiwandani hapo kwa mwaka. Jumla Euro milioni 3.5 sawa na shilingi bilioni tisa zimetumika katika maboresho hayo.