……………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Haki Madini, limewajengea uwezo kwa kuwapa mafunzo ya ujasiriamali wanawake 30 wa vikundi 15 vya Tarafa ya Moipo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Ofisa miradi wa shirika la Haki Madini, Esther Somi akizungumza kwenye kata ya Naisinyai, amesema wajasiriamali hao wamepatiwa mafunzo mbalimbali ya kuendeleza biashara yao.
Somi amesema mara nyingi shirika la Haki Madini, limezoeleka kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo na sasa wamewageukia wajasiriamali.
“Haki Madini pamoja na kuwasaidia wanawake wajasiriamali, bado tutaendelea kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo wa madini nchini,” amesema Somi.
Amesema wanawake hao wajasiriamali wadogo na wa kati wamejengewa uwezo kwa kupatiwa elimu ya fedha na kutunza kumbukumbu.
Alisema kupitia mtu mmoja mmoja au vikundi, wajasiriamali hao wataweza kupiga hatua na kujiendeleza zaidi kiuchumi wakifuatilia kiuhakika mafunzo hayo.
Mmoja kati ya wanufaika wa mafunzo hayo, Mary Lyimo amelishukuru shirika la Haki Madini kwa kuwajengea uwezo na kuomba mafunzo hayo yawe endelevu.
Lyimo amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo zaidi katika shughuli zao za ujasiriamali ili waweze kupiga hatua.
Ofisa maendeleo ya jamii wa mji mdogo wa Mirerani, Isack Mgaya amesema mafunzo hayo yatawasaidia wajasiriamali hao katika biashara zao mbalimbali.
Mgaya amesema Haki Madini wametoa mafunzo hayo Kwa wakati muafaka kwani wajasiriamali hao wamepatiwa mikopo na halmashauri ya wilaya hiyo.
Ofisa miradi wa shirika la Haki Madini, Bernard Njaidi amewapongeza wajasiriamali hao kwa namna walivyoshiriki na kufanikisha mafunzo hayo.
Njaidi amesema wanawake hao wasibaki na elimu waliyoipata ila wanapaswa kuwafundisha wenzao mafunzo waliyoyapata.