Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akifuatilia maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira ( DAWASA) Cyprian Luhemeja, wakati alipofanya ziara kukagua vyanzo vya maji vya Ruvu chini na Ruvu juu ili kukagua hali ya uzalishaji na usambazaji wa maji katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani Novemba 15, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira ( DAWASA) Cyprian Luhemeja, wakati alipofanya ziara kukagua vyanzo vya maji vya Ruvu chini na Ruvu juu ili kukagua hali ya uzalishaji na usambazaji wa maji katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani Novemba 15, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua hali ya uzalishaji na usambazaji wa maji katika vyanzo vya maji vya Ruvu chini na Ruvu juu, mkoani Dar es Salaam na Pwani Novemba 15, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*************************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku tatu kuanzia leo Jumatatu Novemba 15, 2021 kwa wasimamizi wa Bonde la Mto Ruvu wafuatilie njia zote za kuingiza maji katika mto huo ambazo zimechepushwa ziwe wazi ili maji yaweze kuingia na kupunguza changamoto ya upungufu wa maji.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewaagiza wasimamizi wa mabonde yote nchini wasikae maofisini na badala yake wapite katika maeneo yote wanayoyasimamia na wahakikishe yapo salama. “Tumieni sheria iliyoanzisha mamlaka yenu kuhakikisha mnailinda mito na maziwa.”
Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maji itafute chanzo kingine cha maji kitakachosaidiana na Mto Ruvu ili kuhakikisha maji yanapatikana kwa uhakika katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
Ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu Novemba 15, 2021) baada ya kutembelea vyanzo vya maji vya Ruvu Chini na Ruvu Juu ili kukagua hali ya uzalishaji na usambazaji wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam.
“Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo maalumu katika suala zima la upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi hadi washio vijijini, Wizara ya Maji hakikisheni mnatafuta vyanzo vingine ili malengo hayo yatimie.”
Waziri Mkuu alieleza kuwa Mto Ruvu umeathirika na shughuli za kibinadamu zinazochangia maji kupungua, hivyo wahusika wasimamie ipasavyo ili kupunguza tatizo hilo. Amesema idadi kubwa ya mifugo katika maeneo hayo inaathiri chanzo hicho.
Mheshimiwa Majaliwa ameziagiza Wizara za Maji, Maliasili na Utalii, na Mifugo na Uvuvi zikutane na kuona namna bora ya kuboresha mazingira ya ufugaji ili Mto Ruvu ubaki kwa ajili ya kuzalisha maji katika Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakazungumze na wafugaji na waweke utaratibu wa kuratibu shughuli za ufugaji bila ya kuathiri chanzo hicho cha maji. “Mifugo tunaihitali lakini lazima iratibiwe.”
Amesema elimu ya ufugaji bora lazima itolewe kwa wafugaji, mfano mtu mmoja anapopeleka ng’ombe 1,000 kwenda kuwanywesha maji mtoni wanaathiri watu wengi kwani kitendo hicho kinaathiri vyanzo vya maji na kusababisha upungufu.
Naye, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema licha ya Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika mitambo ya kuzalishia maji ya Ruvu Chini na Ruvu Juu ili kuhakikisha wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wanapata maji ya kutosha. “Vyanzo hivyo vina uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 520 huku mahitaji yakiwa ni lita milioni 544.”
Amesema kutokana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi kwa sasa vyanzo hivyo vinazalisha lita milioni 350. Amesema ili kukabaliana na changamoto hiyo Wizara inafikiria kuwekeza katika mradi wa Mto Rufiji ambao utasaidia kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji katika mikoa hiyo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema kwa sasa hali ya uzalishaji wa maji imepungua kutoka lita milioni 520 hadi lita milioni 460 kwa siku.
Amesema kupungua huko kunatokana na sababu mbalimbali zikiwemo za mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na kuwepo kwa makundi makubwa ya mifugo katika eneo la chanzo cha Mto Ruvu.
“Mtambo wa Ruvu Chini ndio ambao umeathirika zaidi kutokana na changamoto ya kupungua kwa kina cha maji katika Mto Ruvu. Kwa sasa, uzalishaji umepungua kutoka lita za ujazo milioni 270 kwa siku hadi lita za ujazo milioni 119.459.”