Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Viongozi wa Baraza la Wahindu Tanzania, wakati akiwasili kwenye siku kuu ya Diwali na sherehe za mwaka mpya wa kihindu, Kisutu jijini Dar es Salaam Novemba 15, 2021. Kutoka kulia ni Rais wa Baraza la Wahindu Tanzania Bavin Borkhataria, Makamu wa Rais wa Baraza la Wahindu Tanzania Jigar Patel na Mkuu wa Mkoa wa Dar ess Salaam Amos Makala.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikaribishwa kimila, wakati akiwasili kwenye siku kuu ya Diwali na sherehe za mwaka mpya wa Kihindu, zilizofanyika, Kisutu jijini Dar es Salaam
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwasha mshumaa, kuashiria kama ishara ya kupokea mwaka mpya wa Kihindu, kwenye siku kuu ya Diwali na sherehe za mwaka mpya wa Kihindu, zilizofanyika, Kisutu jijini Dar es Salaam
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza kwenye siku kuu ya Diwali na sherehe za mwaka mpya wa Kihindu, zilizofanyika, Kisutu jijini Dar es Salaam
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Baraza la Wahindu Tanzania, kwenye siku kuu ya Diwali na sherehe za mwaka mpya wa kihindu, Kisutu jijini Dar es Salaam
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiagana na Rais wa Baraza la Wahindu Tanzania Bavin Borkhataria, kwenye siku kuu ya Diwali na sherehe za mwaka mpya wa kihindu, Kisutu jijini Dar es Salaam Novemba 15, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………
*Ni kutokana na mchango mkubwa inaoutoa katika huduma za jamii
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameipongeza Jumuiya ya Kihindu nchini kutokana na mchango mkubwa inaoutoa kwenye jamii hususan katika utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu, maji, michezo na huduma za kiroho ambazo zimekuwa chachu kwa mshikamano na umoja.
Mheshimiwa Majaliwa amesema sambamba na suala hilo la kiroho, pia Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Shree Hindu Mandal kwa upande wa huduma za afya. “Jambo lililonivutia zaidi kwenye eneo hilo ni Kitendo cha Hospitali zenu kupokea wagonjwa ambao asilimia 95 wanatumia bima ya afya ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).”
Mheshimiwa Majaliwa alitoa kauli hiyo jana usiku (Jumapili, Novemba 14, 2021) wakati alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya siku ya Diwali inayoashiria kuanza kwa mwaka mpya wa Kihindu 2078 (Vikram Samvat 2078) yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Patel Samaj, Kisutu mkoani Dar es Salaam.
“Kama mnavyofahamu, Serikali ina lengo la kuongeza wigo wa matumizi ya bima ya afya kupitia Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote. Hatua za awali kuhusu Mpango huo zimekamilika na katika bajeti ya Serikali mwaka wa fedha 2022/2023, Mheshimiwa Rais Samia ameruhusu kutenga jumla ya shilingi bilioni 149.7 kwa ajili ya mpango huo”.
Pia, Waziri Mkuu ameihakikishia Jumuiya ya Kihindu Tanzania kuwa Serikali inaendelea kuheshimu uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania na itaendelea kushirikiana nao pamoja na taasisi nyingine za kidini kwa ajili ya ustawi wa Taifa na watu wake.
“Serikali inapongeza na kuthamini mchango wenu katika kujenga jamii yenye kutii mamlaka na sheria za nchi. Nitoe rai kwenu kutumia vema fursa ya uwepo wa kamati za amani kujadili pamoja na kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa na amani na utulivu.”
Alisema huduma ya kiroho imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha amani, umoja na mshikamano nchini. “Nitumie fursa hii kuipongeza tena Taasisi ya Shree Sanatan Dharma Sabha kwa kuwekeza nguvu kubwa kwenye mafunzo ya kiroho hususan kwa Jamii ya Wahindu nchini.”
“Elimu mnayoitoa inawafikia vizuri waumini na wanaizingatia. Nataka niwakumbushe tena viongozi wote wa dini neno lenu ni muhimu sana, viongozi wa dini mnaaminiwa sana na ndiyo kwa sababu Serikali inaendelea kuwaahidi kuwapa ushirikiano katika kusimamia mwenendo shughuli zenu na haitaingilia ila itashirikiana nanyi.”
Aidha, Waziri Mkuu ameitaka jamii hiyo na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuimarisha mshikamano ambao umejengwa kwa muda mrefu, wazidishe utu tulio nao, sambamba na kuwajali wajane na watu wengine wenye uhitaji.
Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Wahindu Tanzania Bhavin Borkhataria alitumia fursa hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia kwa jitihada zake za kuiletea nchi maendeleo na kwamba wataendelea kumuunga mkono.
Pia, kiongozi huyo aliiomba Serikali isaidie Baraza la Wahindu Tanzania liweze kutambuliwa kwenye Gazeti la Serikali kwa kuwa ndiyo chombo chenye maamuzi ya juu kwa Taasisi zote za kihindu zilizopo nchini.