********************************
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania inaandaa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza (UK – Tanzania Business Forum) litakalofanyika tarehe 16 Novemba, 2021 katika ukumbi wa mikutano wa JNICC jijini Dar es Salaam, ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kongamano hili linaratibiwa kwa pamoja kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji na Wizara ya Viwanda na Biashara na linalenga kujadili fursa za biashara ili kuongeza biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili, kutatua changamoto katika ufanyaji biashara ili kuhakikisha fursa za biashara zinafunguliwa, kujadili miradi inayoendelea kutekelezwa yenye fursa za kupatiwa wawekezaji na kusaidia Kampuni za Tanzania kuingia katika soko la Uingereza. Sekta za kipaumbele zitakazohusika kwenye kongamano hili ni kilimo, Madini, Nishati, Uchumi wa Bluu na Miundombinu.
Kongamano hilo litahusisha washiriki zaidi ya 200 ambapo tunatarajia kuwa na kampuni 30 kutoka Uingereza, kampuni 150 za Uingereza na Tanzania zilizopo nchini na Wizara na Taasisi za Serikali kutoka Tanzania bara na Zanzibar, taasisi za sekta binafsi zinazohudumia wawekezaji (TPSF, TCCIA na CTI) na Maafisa wa Serikali ya Uingereza wanaoshughulikia masuala ya Biashara.
Pamoja na Kongamano hilo, kutafanyika Mkutano wa majadiliano kati ya Serikali ya Tanzania na Uingereza (G2G) ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji inaratibu maandalizi yake. Majadiliano hayo yatajikita kwenye Maboresho ya mazingira ya Biashara ikiwemo utekelezaji wa mpango wa Blue print, Usimamizi wa Kodi na Utulivu wa Sera na Sheria zinazogusa biashara na uwekezaji. Baada ya majadiliano hayo pande hizo mbili zitasaini maeneo ya ushirikiano ya utekelezaji wa masuala yatakayoafikiwa ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.