Na Mwandishi wetu, Mirerani
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Manyara, RAS Caroline Mthapula ametaja hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi mkubwa wa madini ya Tanzanite katika eneo la Mirerani Tanzanite City Wilayani Simanjiro.
RAS Mthapula akizungumza hivi karibuni na ujumbe ulioongozwa na Makatibu Wakuu wa Wizara nane ametaja kazi zilizofanyika ni upangaji, upimaji na uchoraji wa miundombinu muhimu katika eneo la ekari 30 kati ya ekari 250 iliyofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakisaidiana na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro.
“Majengo yaliyochorwa ni pamoja na majengo madogo ambayo yalitarajiwa kujengwa na wadau wa madini ya Tanzanite kwa mkataba maalum wa ujenzi baina yao na Halmashauri jengo la Mirerani Tanzanite Trading Center ambalo litakodishwa kwa wafanyabiashara, jengo la shopping mall ambalo litakodishwa na ofisi zikiwemo za Wizara ya Madini na polisi,” amesema RAS Mthapula.
Amesema TARURA wamesafisha eneo la ujenzi wa soko na kuweka kivuko kimoja, wamechonga barabara ndani ya ekari 30 na kuweka mkuza kuzunguka ekari 250 kwa ajili ya ulinzi.
“Shughuli zilizobaki ni pamoja na kuweka moram na kuweka mfereji, tunaishukuru Wizara ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na TARURA wameshatoa fedha kwa ajili ya kukamilisha kazi zilizobaki,” amesema RAS Mthapula.
Amesema kazi ya uwekaji miundombinu ya maji na kuvuta maji hadi eneo la mradi imefanywa vizuri na RUWASA inasubiri usambazaji ufanyike pindi majengo yakikamilika.
Amesema uwekaji wa miundombinu ya umeme umefanyika vizuri kupitia TANESCO kwani nguzo zimefika eneo la mradi na wanasubiri kumalizika kazi baada ya ujenzi wa majengo kuanza.
Amesema eneo la ujenzi wa jengo la soko la madini limeshasafishwa na mchoro tayari upo na Wizara ya Fedha na Mipango tayari imeshaandaa fedha za ujenzi wa soko na jengo litajengwa na mkandarasi na atalipwa kadiri atakavyowasilisha cheti, kazi inayoendelea kwa sasa ni kukamilisha utaratibu wa kumpata mkandarasi.
“Mradi huu wa ujenzi wa soko la madini utakapokamilika tunatarajia utasadia kuongeza kipato kwa wananchi wa eneo la Mirerani, vijiji vya jirani, Wilaya ya Simanjiro na Mkoa wa Manyara kwa ujumla kwa kupata fursa ya kufanya biashara ndogo ndogo na za kati,” amesema RAS Mthapula.
Amesema Serikali na Halmashauri ya Wilaya zitapata mapato yatakayotokana na minada ya madini itakayofanyika na kuongezeka kwa mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro kutokana na kukodisha eneo la soko, service leavy na tozo ya kuongeza thamani ya madini.
“Kuongeza ajira kwa wananchi katika eneo la mji wa Mirerani, kuongeza ubora wa huduma za kijamii kutokana na CSR, mji wa Mirerani na Tanzania kwa ujumla kujulikana na kutambulika kimataifa kuwa ni chanzo pekee cha madini ya Tanzanite duniani na kuongezeka kwa miundombinu mbalimbali ya kihuduma na malazi katika eneo la mji mdogo wa Mirerani,” amesema RAS Mthapula.