………………………………………………
Na.Joctan Agustino,NJOMBE
Jopo la mawakili 20 lililoundwa na mkuu wa wilaya ya Njombe ili kutoa usaidizi na utatuzi wa changamoto za kisheria katika masuala mbalimbali ikiwemo mirathi,Ndoa,ardhi na nyinginezo limepokea mamia ya wananchi wakilalamikia kuzurumiwa haki zao .
Awali mkuu wa wilaya ya Njombe Kisa Gwakisa Kasongwa akiweka bayana sababu ya kuandaa tamasha la siku tatu la kusikiliza kero za wananchi amesema ni kutokana na idadi kubwa ya watu wanaofika ofisini kwake wakilalamikia kupokwa mali za urithi ,migogoro ya ardhi na ndoa jambo ambalo likamfanya kuona ulazima wa kuandaa siku itakayowakutanisha wahanga na wanasheria ili kupata suluhisho la changamoto zao.
Kasongwa amesema tamasha hilo la siku tatu limebeba dhima nne ambazo ni kusikiliza kero za wananchi,Kuhamasisha utalii ,kuhamasisha wananchi kupiga chanjo pamoja na kumshukuru mama Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mabilioni ya fedha katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani humo.
Katika hatua nyingine mkuu wa wilaya ya Njombe ametembelea na kukagua banda la mfuko wa hifadha ya jamii wa NSSF na kisha kuonyesha kuridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wa majukumu yake na kisha kutoa rai kwa makampuni kuhakikisha yanapeleka michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Makambako Deo Sanga maarufu Jah Pipo amesema kitendo kilichofanywa na mkuu wa wilaya ya Njombe kuandaa tamasha kubwa la kusikiliza kero za wananchi ni kitendo cha kihistoria na kwamba elimu ya kisheria wanayopata wananchi kutoka kwa mawakili 20 itakuwa na mafanikio makubwa
Kuhusu haki za wafanyakazi Deo Sanga amesema kuna makampuni mengi hayapeleki michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii na kwamba wakati umefika kwa taasisi zenye dhamana ikiwemo NSSF kuyafata makampuni na kisha kuwaunganisha wafanyakazi katika mifuko hiyo.
“Makampuni yanapaswa kuwaunganisha wafanyakazi wake na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kupata stahiki za uzeeni baada ya kustaafu kazi”Alisema Deo Sanga mbunge wa Makambako.
Nae mkuu wa mkoa wa Njombe mhandisi Marwa Rubirya wakati akifanya uzinduzi wa tamasha hilo la siku tatu amesema limekuja katika kipindi sahihi kwasababu Njombe imekuwa na mikasa mingi ya migogoro ya ardhi,Mirathi na Ndoa hivyo wananchi wajitokeze kueleza kero zao.
“Hatua hii ni utekelezaji wa maagizo ya rais hivyo nampongeza mkuu wa wilaya kwa uthubutu na ubunifu mkubwa uliyofanywa kwasababu njombe inatakwimu nyingi za migogoro ya ardhi”Alisema mkuu wa mkoa wa Njombe mhandisi Marwa Rubirya .
Baadhi ya wananchi waliyojitokeza kuwasirisha kero zao mbele ya mkuu wa wilaya ni Jane Mkungilwa ambaye anasema yeye ameporwa ardhi tangu mwaka 2017 hivyo aliposikia uwepo wa tamasha hilo akalazimika kufunga safari kutoka Ikelu iliyopo kata ya Mtwango kuja kufata huduma na usaidizi wa kisheria.
“Kesi yangu ilishafika mahakamani na kumalizika lakini pamoja na hatua hiyo bado eneo langu sijalipata hivyo tunaomba kusaidiwa kupata haki zetu sisi wanyonge” Alisema Jane Mkungilwa.
Tamasha hilo lililopewa jina la Njombe ya Mama Samia limeanza leo desemba 15 na linatarajiwa kuhitimishwa desemba 17.