Na Joseph Lyimo, Hanang’
ELIMU ya haki ya afya ya uzazi kwa wasichana na wanawake wa Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, iliyotolewa hivi karibuni, imeanza kuonyesha matokeo chanya kwa makundi rika ya eneo hilo.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Endasak wamenufaika na mradi huo wa elimu hiyo ya afya ya uzazi kwa kuwakomboa na kuepuka kuzaa bila mpango na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya.
Elimu hiyo ilitokana na mradi uliotekelezwa hivi karibuni na Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Manyara (MNRPC) kwa ufadhili wa shirika la Women Fund Tanzania Trust (WFT).
Mkazi wa kata ya Endasak, Faudhia Ally amesema elimu hiyo waliyopatiwa imewabadili kwani ni nzuri na imewasaidia kujiunga na uzazi wa mpango na yeye binafsi anawafundisha wenzake.
Faudhia amesema amewashauri wenzake kujiunga na uzazi wa mpango hivyo kuepuka mimba zisizotarajiwa ambazo awali ilikuwa tatizo kwa wasichana wa eneo hilo.
“Huwa naenda zahanati au kituo cha afya kila baada ya miezi mitatu kwa ajili ya kuchoma sindano ya uzazi wa mpango na ninapewa ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya,” amesema.
Mwanamke mwingine wa eneo hilo Magreth Ombay amesema tangu alipopata elimu ya mradi huo ameweza kutoa elimu kwa watu wengine hivyo kupunguza wimbi la watoto kutelekezwa.
Amesema wanaishukuru Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Manyara (MNRPC) kwa kuwafikishia mradi huo kwani wengi wamenufaika kutokana na elimu waliyoipata.
“Hata mimba zisizotarajiwa hivi sasa hatuzioni tena kama awali kwani wasichana na wanawake wengi wamejitambua na kuepuka kufanya mapenzi bila kinga,” amesema Ombay.
Muuguzi msaidizi wa hospitali ya wilaya ya Hanang’ ya (Tumaini) Anasia Mariki anasema wanawake na wasichana waliopata elimu hiyo wanaofika kupata huduma wameanza kuchukua hatua kwa kubadili mtazamo.
Mariki amesema baada ya wanawake hao kujiunga na uzazi wa mpango kuna maudhi madogo madogo yanawapata ila hayana madhara kwani ni mabadiliko ya kawaida.