Afisa Habari wa Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma Hassan Mabuye akiongea na wakazi wa kata ya Ihumwa jijini Dodoma kuhusu madhara ya ujenzi bila kufuata taratibu za mipango miji wakati wa kampeni ya mtaa kwa mtaa kuhusu elimu ya sekta ya ardhi, kushoto ni Afisa Habari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Moses Mpunga.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Nkuhungu jijini Dodoma wakipata elimu kupitia machapisho kutoka kwa mtoa elimu katika kampeni ya elimu ya mtaa kwa mtaa kuhusu sekta ya ardhi Shabani Migongano.
Gari maalumu linalotumika katika kampeni ya elimu ya sekta ya ardhi mtaa kwa mtaa katika jiji la Dodoma lilioandaliwa na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Chang’ombe jijini Dodoma wakifuatilia kwa karibu matangazo ya kampeni ya elimu ya ardhi mtaa kwa mtaa.
Mtoa elimu katika kampeni ya mtaa kwa mtaa kuhusu sekta ya ardhi Shabani Migongano akigawa machapisho mbalimbali kwa wakazi wa Kata ya Nzuguni jijini Dodoma.
Mkazi wa Nkuhungu jijini Dodoma Bibi Fatma Msham ambaye ni muendesha bajaji akipokea elimu kwa njia ya machapisho kutoka kwa mtoa elimu Bibi Asma Khassim.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Nzuguni jijini Dodoma wakifuatilia kwa karibu matangazo ya kampeni ya elimu ya ardhi mtaa kwa mtaa.
*************************
Na. Ramadhani Juma na Hassan Mabuye Dodoma
OFISI ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma wanafanya kampeni ya kutoa elimu kwa umiliki wa ardhi Jiji la Dodoma kwa kupita katika mitaa ya jiji hilo na kukutana na wananchi kwenye maeneo yao na kuwapa tahadhari kuhusu ujenzi bila vibali ili kuepuka usumbufu wakati wa ujenzi.
Kampeni hii ambayo inaendeshwa kwa kuwapatia elimu kwa njia ya mazungumzo, matangazo, sanaa za maagizo, nyimbo za asili, pamoja kugawa vipeperushi vinavyoelezea masuala mbalimbali yahusuyo arhi ikiwemo vibali vya ujenzi na kodi za pango la ardhi.
Lengo la kampeni hiyo ni kumfikishia mwananchi hususan mkazi wa Jiji la Dodoma elimu kuhusu umiliki wa ardhi, ujenzi kwa kufuata taratibu za mipango miji kodi ya pango la ardhi na fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye sekta ya ardhi ikiwemo upatikanaji wa viwanja vya makazi na uwekezaji wa viwanda katika jiji la Dodoma.
Afisa Habari wa Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma Hassan Mabuye alisema kampeni hiyo kwa awamu ya kwanza inafanyika kwa muda wa siku tano mfululizo na inatajiwa kukamilika Jumatatu Novemba 15, 2021.
Mabuye alisema zoezi la kuwafuata wananchi katika maeneo yao na kuwapatia elimu hiyo kuhusu masuala mbalimbali ya ardhi ni endelevu na hapo baadaye itafanyika katika wilaya zote za Mkoa wa Dodoma.
“Mpaka sasa tumeshazunguka na kutoa elimu hii katika maeneo kadhaa ya jiji la Dodoma kama Ihumwa, Nzuguni, Chang’ombe, Nkuhungu, Majengo, Mnadani Swaswa, Ilazo, Kikuyu, Chidachi, Makulu na Mnada wa Kizota na muitikio ni mkubwa sana na bado tunaendelea katika maeneo mengine yote ya mkoa wa Dodoma na k tunataraji kufika hadi vijijini” alisema Mabuye.
Alitoa wito kwa wakazi wa jiji la Dodoma kujitokeza kwa wingi pale ambapo kunafanyika mikutano hiyo katika maeneo yao ili kupata elimu hiyo ambapo kwa siku ya leo jumatatu ya Novemba 15, 2021 inataraji kuendelea katika maeneo ya Makulu, Kikuyu na Mjini kati.
Kwa upande wake Afisa Habari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Ramadhani Juma alisema fursa ya Jiji hilo ya kushirikiana na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma inawasaidia kuwaelimisha wakazi wa jiji hilo kuhusu masuala ya ardhi na kwamba itawasaidia kupunguza changamoto kadhaa za uelewa kwa wananchi kwani wanapata fursa pia ya kuuliza maswali kwa mambo yanayowatatiza.
“Lakini pia tunawatangazia uwepo wa fursa za upatikanaji wa viwanja vinavyouzwa na Halmashauri kwa ajili ya matumizi mbalimbali katika maeneo ya jiji hilo ikiwemo eneo maalum la uwekezaji wa viwanda kwenye Kata ya Nala ambapo tayari baadhi ya wawekezaji wameanza ujenzi wa viwanda kama kiwanda kikubwa cha mbolea Afrika Mashariki ambacho tayari ujenzi wake umeanza.
Aidha, Juma alisema katika mikutano hiyo na wananchi pia wanawakumbusha wale ambao walishanunua viwanja siku za nyuma na bado hawajakamilisha malipo ya viwanja hivyo kufanya hivyo hadi kufikia Novemba 30, 2021 kwani baada ya hapo vitauzwa upya kwa wateja wengine bila mteja wa awali kupewa taarifa.
Aliyataja baadhi ya maeneo ambayo wateja wengi hawajakamilisha malipo ya viwanja kuwa ni pamoja na Mtumba, Kikombo, Nzuguni, Iyumbu, Njedengwa, Michese, Mkalama, Nala, Michese, Wia, na Mahomanyika.