Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, akizungumza wakati wa kufunga Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam, ambapo amewataka wataalamu wa masuala ya fedha kuendelea kutoa elimu kwa Umma.
Afisa Mkuu wa Tathmini ya Mikopo wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Bw. George Nyamrunda akitoa maelezo ya huduma zinazotolewa na benki hiyo kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, alipotembelea banda hilo wakati wa kufunga Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Charles Mwamwaja akizungumza wakati wa kufunga Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, Maadhimisho hayo yamefungwa na Katibu mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, akizungumza jambo alipotembelea banda la Benki ya TIB, wakati wa kufunga Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja Masoko na Masuala ya Biashara wa Benki ya TIB, Bw. Said Mkabakuli.
Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa. Kulia waliokaa ni Katibu Tawala wa mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Hassan Rwaga, kulia kwa Katibu Mkuu ni Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Charles Mwamwaja.
Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, akifurahia jambo na Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Charles Mwamwaja baada ya kufunga Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.
****************************
Na Josephine Majura, WFM, Dar es Salaam
Serikali imetoa wito kwa Washiriki waliohusika na utoaji wa elimu kwa Umma katika Maadhimisho ya kwanza ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa kuendelea kutoa elimu ili kuwezesha watanzania wengi zaidi kuwa na uelewa wa masuala ya elimu ya fedha ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba wakati akifunga Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
“Naomba tuendelee kushirikiana na wadau mbalimbali wa Sekta ya Fedha katika kuhakikisha malengo ya Maadhimisho haya yanafikiwa hususan kwa watu ambao kwa namna moja au nyingine hawakupata fursa ya kuhudhuria maadhimisho haya alisema Bw. Tutuba”.
Aidha Bw. Tutuba alisema kuwa ili kuhakikisha elimu inawafikia wananchi wote Serikali kupitia wizara hiyo imeandaa utaratibu wa kutoa elimu kwa njia ya makundi ambapo itakua na Siku ya Elimu ya Fedha kwa Watoto, Wanawake, Vijana na Wajasiriamali Wadogo pamoja na Elimu ya Fedha kwa Viongozi wa Kisiasa katika ngazi mbalimbali, Wahariri, Wastaafu na wengineo.
Alifongeza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika Sekta ya Fedha na kuendelea kufanyia kazi changamoto mbalimbali katika sekta hiyo ikiwemo masuala ya riba katika mabenki kuhakikisha zinakua rafiki kwa wananchi ili waweze kunufaika na sekta hiyo ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi na Taifa kwa ujumla.
Bw. Tutuba alimshukuru Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, ambaye alifungua Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa siku ya Jumatano, tarehe 10, Novemba 2021 na kuwashukuru wote waliohudhuria maadhimisho hayo pamoja na Timu ya Wataalam iliyofanya maandalizi na kuwezesha kufanyika kwa maadhimisho hayo.
Kwa upande wake Kamishna wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha nchini Dkt. Charles Mwamwaja, alisema kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Huduma Ndogo za Fedha Kitaifa yamefanyika ikiwa ni utekelezaji wa Programu yake ya Uelimishaji Umma ya Miaka mitano (National Financial Education Programme; 2020/21-2025/26).
Aliongeza kuwa wizara itaendelea kutoa elimu ya masuala ya fedha kwa umma ili kuongeza uelewa na weledi kwa umma kuhusu huduma za fedha zinazotolewa ili kujenga uchumi na kuondoa umasikini.
Kwa upande wao washiriki wa maadhimisho hayo ikiwemo Benki, Taasisi za Bima, Masoko ya Mitaji na Dhamana, Mifuko ya Jamii na Huduma ndogo ya Fedha, wameipongeza wizara kwa kuandaa maadhimisho hayo kwa kuwa wameweza kujifunza mambo mbalimbali ambayo yatasaidia kukuza sekta hiyo.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, yaliyofanyika kwa siku saba katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam yamekamilika leo, ambapo maadhimisho mengine yanatarajiwa kufanyika mwakani mwezi Novemba.