Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku akibadilisha mawazo na Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Saady Khimji, Mratibu wa MNLMI, Miraji Magai kulia. Kushoto ni Mhadhiri wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Dk.Beatrice Mkunde.
Na Mwandishi Wetu
KATIKA kuhakikisha amani, umoja na maendeleo katika Serikali za Mitaa yanapatikana madiwani, watendaji wa kata, mitaa, wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji wametakiwa kuzingatia sheria, maadili, uadilifu katika kutekeleza majukumu yao.
Hayo yamesemwa na Mhadhiri wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Dk. Beatrice Mkunde mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, wakati akitoa mada kwenye mdahalo wa amani uliondaliwa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) na Taasisi ya Kimataifa ya Republican (IRI) kwa viongozi hao.
Katika mdahalo Dk. Mkunde aliwasilisha mada mbili ambazo ni tushirikiane, kudumisha na kuimarisha, udugu, uzalendo, uwajibikaji, amani, maridhiano na maendeleo na mvutano kati ya demokrasia na maadili na jukumu la wadau kudumisha maadili ya taifa.
Alisema taasisi ya MNF imelenga kushiriki kupigania amani, umoja na maendeleo hivyo ni jukumu la viongozi hao kuwa na maadili kufanikisha hayo malengo ili jamii ifanikiwe.
“Uwepo wa maadili katika majukumu yetu utachochea uvumilivu wa kidini, kisiasa, kikabila na kila jambo hivyo lengo la amani, umoja na maendeleo litaonekana kwa vitendo,” alisema.
Dk. Mkunde alisema mitaa, vijiji na vitongoji ndio maeneo ambayo yanaonesha mafanikio ya nchi kwa kila sekta hivyo anawaomba viongozi wa ngazi hiyo kutekeleza majukumu yao kwa kuweka maslahi ya taifa mbele na sio maslahi binafsi.
Alisema iwapo jamii itakuwa na amani, umoja na maendeleo ni wazi kuwa lengo la muasisi wa MNF Hayati Mwalimu Julius Nyerere la kuona Tanzania inapiga hatua kwa kila sekta litaonekana.
Aidha, mhadhiri huyo alisema watendaji na madiwani wanapaswa kusimamia miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa katika maeneo yao kwa kuwa ni moja ya majukumu yao kisheria na kikatiba.
“Serikali za mitaa ni nguzo muhimu sana katika kujenga amani, umoja na maendeleo ndio maana hata Hayati Nyerere alivyoifuta alikuja kujuta na kuirejesha tuitumie kuchochea mabadiliko nchini,” alisema.
Mkunde alisema amani ni dhana pana ambayo inahusu uhakika wa chakula, uhuru, maendeleo, uchumi na kwamba isichukuliwe kukosa amani ni kukuwepo vita.
Kwa upande wake Mzee Galius Abeid kutoka MNF, alisema ili kuiona amani ya kweli ni lazima viongozi hao kutenda haki kwani haki ni tunda la amani.
“Amani ni ibada, sala na upendo hivyo nitumie nafasi hii kuwaomba kusimamia hilo kwani hayo maadili mnayoambiwa kuyatekeleza yatatokana na uwepo na utendaji wa haki kwa jamii zenu,” alisema.
Awali akifungua mdahalo huo, Mkurugenzi wa MNF Joseph Butiku alisema taasisi hiyo imeamua kujikita kwenye mazungumzo na viongozi na wadau mbalimbali kuhakikisha amani na umoja wa Tanzania unakuwa endelevu.
Butiku alisema kwa siku za karibuni kulianza kutokea viashiria vya uvunjifu wa amani hivyo katika kuhakikisha hali hiyo haitokei wameona ni vema kuwapa nafasi makundi yote ambayo kwa njia moja au nyingi yanahusika kulinda amani.
“Tunazungumza na makundi yote kuanzia ngazi ya vijiji hadi taifa lengo likiwa ni kupeana nafasi sisi Watanzania kujadiliana amani, umoja na maendeleo yetu pamoja,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema Tanzania ni nchi ambayo inaendeshwa kwa mfumo wa vyama vingi hivyo ni lazima kukaa pamoja na kujadiliana namna ya kufika pamoja bila kukwazana.
Diwani wa kata ya Vijibweni wilayani Kigamboni, Zakaria Mkundi alisema mdahalo huo una tija kwao kwa kuwa unarejesha maadili na uadilifu kwa nchi na watumishi.
Mkundi alitoa rai kwa MNF kuendelea kutoa mafunzo kwa viongozi ili waweze kujisahihisha kama ambavyo Hayati Nyerere alitamani.
Naye Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam Saady Khimji alisema mafunzo hayo yamemuongezea uelewa wa namna ya kufanya kazi kwa weledi na watendaji wa Serikali tofauti na alivyokuwa awali.
“Mimi naamini tukitokea hapa lazima tuoneshe tofauti katika majukumu yetu ili kuweza kuchochea amani, umoja na maendeleo katika maeneo yetu na nchi kwa ujumla,” alisema.
Naibu Meya huyo alisema kupitia mafunzo hayo amebaini kuwa kila mtendaji na kiongozi wa kisiasa akiamua kutekeleza majukumu yake kisheria na taratibu changamoto na malamiko ya wananchi yatapungua.
Diwani wa Kisukulu CCM, Lucy Lugome alisema katika kufanikisha dhana ya amani, umoja na maendeleo ni lazima watendaji na viongozi wa kisiasa kuacha kuweka maslahi yao mbele.