******************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
KAMPUNI ya Tanzanite Forever Lapidary LTD yenye ofisi Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, inajivunia kuwa kampuni ya kwanza ya madini kushinda tuzo ya kulipa mrabaha Serikalini.
Mkurugenzi wa kampuni ya Tanzanite Lapidary Forever, Faisal Juma Shabhay amesema hatua hiyo inawapa nguvu na ari zaidi ya kufanya kazi kwenye sekta hiyo ya madini ya Tanzanite.
Faisal ni mbia wa kampuni ya Sky Associates Group, iliyokuwa inamiliki kampuni ya TanzaniteOne iliyokuwa na leseni ya eneo la kitalu C na kuchimba madini ya Tanzanite.
Faisal amesema ni hatua kubwa kwa kampuni hiyo kuwa ya kwanza na kupata tuzo kwa kuongoza kwa kulipa mrabaha kwenye madini ya Tanzanite.
Amesema wanafanya biashara kwa utaratibu uliwekwa na serikali kwa weledi, ili zao la Tanzanite lizidi kupiga hatua zaidi kimataifa.
“Nia yetu ni zao hili la madini ya Tanzanite liwe na bei kubwa duniani na kuwanufaisha wadau wote wa Tanzanite na Taifa kwa ujumla na kuwa brand (bidhaa) bora zaidi,” amesema Faisal.
Wakatibu wakuu wa wizara nane walitembelea ofisi ya Tanzanite Forever Lapidary Ltd na kupongeza uandaaji na uongezaji thamani madini ya Tanzanite unavyofanyika.
Katibu Mkuu wa wizara ya madini, Profesa Simon Msanjila amesema kampuni ya Tanzanite Forever Lapidary Ltd ni miongoni mwa makampuni ya mwanzo kutekeleza agizo la serikali kuhamia Mirerani.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Caroline Mthapula amesema hadi sasa wanunuzi wakubwa 45 wamefungua ofisi ya kununua madini ya Tanzanite baada ya agizo la serikali la biashara ya Tanzanite kufanyika Mirerani.
Katibu mkuu wa wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, Mary Makondo amepongeza wanawake wa kampuni ya Tanzanite Forever Lapidary Ltd wanavyojihusisha kufanya kazi kwenye sekta ya madini ya Tanzanite.