Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali yatakayofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 12 Desemba, 2021 kwenye viwanja vya Rock City Mall, Jijini Mwanza.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Prof. Jamal Katundu wakati mkutano huo uliofanyika Novemba 13, 2021 Jijini Dodoma.
Sehemu ya waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama wakati wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Bunge, Jijini Dodoma.
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
……………………………………………………..
Na:Alex Sonna,Dodoma
Tanzania itakuwa mwenyeji wa Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali yatakayofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 12 Desemba, 2021 kwenye viwanja vya Rock City Mall, Jijini Mwanza.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati wa mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika katika ukumbi wa Bunge, leo Novemba 13, 2021 Jijini Dodoma.
Waziri Mhagama alieleza kuwa, Maonesho hayo ya Nguvu Kazi au Jua Kali yamekuwa yakijulikana hivyo kwa sababu yanawalenga wajasiriamali wa kati na wadogo waliopo katika sekta isiyo rasmi na lengo kubwa la maonesho haya ni kuwawezesha wajasiriamali kurasimisha shughuli zao kwa kuwapatia fursa ya kutangaza bidhaa zao, kubadilishana taarifa, kukuza ujuzi, kukuza masoko ya bidhaa na kukuza teknolojia ya utengenezaji wa bidhaa pamoja na kuongeza fursa za ajira za staha nchini.
“Tanzania imekua mwenyeji wa maonesho haya mara tano na mwaka huu 2021 itakuwa ni mara ya sita ambapo maonesho hayo yatafanyika Mkoani Mwanza,” alieleza Waziri Mhagama
“Kwa kutambua umuhimu wa maonesho haya tunategemea kuwa na zaidi ya Wajasiriamali 1,000 kutoka Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda, Sudan ya Kusini na Tanzania ambao watashiriki katika maonesho haya ambapo Tanzania itawakilishwa na Wajasiriamali zaidi ya 450,” alisema
Alisema kuwa, Serikali imeendelea kuhakikisha haiwaachi nyuma Wajasiriamali na imekuwa ikiwawezesha kushiriki katika Maonesho mbalimbali ya Kimataifa ikiwemo hayo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kwa jina la Jua Kali au Nguvukazi.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imejipanga kufanikisha maonesho haya kwa lengo la kuwawezesha wajasiriamali wakiwemo vijana, wanawake na wenye ulemavu wanatumia fursa hii kutafuta masoko katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Waziri Mhagama
“Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025 kupitia Ibara ya 26 imeilekeza Serikali kuwezesha wajasiriamali na makundi yao ili waweze kujiajiri na kuajiri wengine,” alisema
Akizungumzia historia ya Maonesho hayo alieleza kuwa, onesho la Nguvu Kazi au Jua Kali hufanyika kila mwaka katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Desemba kama sehemu ya kumbukumbu ya kuanzishwa tena Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Wajasiriamali wadogo na wa kati nchini ni vyema wakatumia fursa ya maonesho haya ili waweze kujifunza mbinu za kutengeneza bidhaa na kutafuta masoko kutoka kwa wenzetu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema
Aliongeza kuwa, Maonesho hayo hufanyika sambamaba na makongamano ya kuwajengea uwezo Wajasiriamali kuhusu masoko, ubora wa bidhaa, urasimishaji biashara na kuongeza thamami ya bidhaa. Pia, maonesho hayo yanaenda sambamba na maadhimisho ya miaka Sitini 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, hivyo alihimiza Vijana wajasiriamali kutumia fursa hiyo kuonesha kazi zao za ubunifu katika sekta ya teknolojia ya habari, viwanda, kilimo, biashara, na huduma za kijamii ikiwemo elimu na afya.
Waziri Mhagama alifafanua kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwezeshaji – Zanzibar, Wizara, Taasisi nyingine za Serikali, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali (CISO) imeunda Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu maandalizi ya Maonesho hayo na fomu za maombi pamoja na maelekezo kwa Wajasiriamali wanaokusudia kushiriki maonesho hayo zinapatikana kupitia Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya/Miji/Manispaa/Majiji kote nchini, Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali (CISO) na katika tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu www.pmo.go.tz.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa wito kwa wadau wote kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kufanikisha maonesho hayo. Pia alitumia fursa hiyo kuhimiza Shirika la Viwanda vidogo (SIDO) kuendelea kusaidia na kuwaibua Wajasiriamali mahiri kushiriki maonesho hayo.
“Nitumie fursa hii kuwasihi wajasiriamali kujitokeza kwa wingi kushiriki maonesho haya bila wasiwasi wowote kwa kuwa tumejipanga kuhakikisha masuala ya afya yanazingatiwa wakati wote wa maonesho hususan tahadhari dhidi ya changamoto ya UVIKO – 19,” alisema