***********************************
Na WAMJW-ARUSHA
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezindua mkakati wa Taifa wa kuzuia magonjwa yasiyoambukiza utakaosaidia kutoa elimu juu ya njia za kupambana dhidi ya magonjwa hayo zikiwemo kufanya mazoezi, kula vyakula vya gharama nafuu visivyochangia kuleta magonjwa hayo kama kama inavyoelekezwa na wataalamu, kuepuka matumizi ya vileo kupita kiasi na mambo mengine yanayoelimishwa na wataalamu.
Uzinduzi huo umefanywa leo Jijini Arusha na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima na kuhudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulika na masuala ya Afya OR TAMISEMI Dkt. Grace Magembe pamoja na Wadau kutoka Taasisi mbali mbali za Serikali na zisizo za Serikali.
Dkt. Gwajima amesema, Magonjwa yasiyoambukiza yanachangia zaidi ya vifo milioni 41, ambayo ni sawa na asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 Duniani vilivyotokea mwaka 2016, hii ni kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za Mwaka 2016.
“Takwimu za Shirika la Afya Duniani za Mwaka 2016 zinaonesha kuwa Magonjwa yasiyoambukiza yanachangia zaidi ya vifo milioni 41, ambayo ni sawa na asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 Duniani vilivyotokea mwaka 2016. Hali hii inatishia ustawi wa maendeleo ya mwanadamu.” Amesema Dkt. Gwajima.
Aliendelea kusema kuwa, magonjwa yasioambukiza yalikuwa yanachangia asilimia 20 tu miaka ya 90 lakini kwa sasa yanachangia asilimia 33 na inakadiriwa yanaweza kufikia hadi asilimia 40 katika baadhi ya maeneo nchini, alisisitiza.
Hata hivyo Dkt. Gwajima amesema kuwa, jambo linalotia hofu ni kuwa katika jamii zetu magonjwa haya yanaanza mapema zaidi na hivyo kuzorotesha nguvu kazi na kusababisha vifo katika umri chini ya miaka 60.
Aidha, ameweka wazi kuwa, Inakadiriwa kuwa katika kipindi cha miaka 20, kuanzia mwaka 2013 gharama zitokanazo na magonjwa haya Duniani zitafikia Dola za Marekani trilioni 47, fedha ambazo zingeweza kutumika kupunguza umaskini kwa watu bilioni 2.5 kwa miaka 50.
Kwa nchi za uchumi wa kati na chini, magonjwa haya yatayagharimu Mataifa hayo jumla ya Dola za Marekani, trilioni 7 kwenye kipindi cha 2011 – 2025, na kuweka wazi kuwa, gharama hizo zinatokana na huduma za matibabu na nguvu kazi inayopotea. Aliendelea kusisitiza Dkt.Gwajima.
Mbali na hayo, amesema kuwa, makadirio yanaonesha kuwa, gharama za huduma kwa magonjwa yasiyoambukiza itafikia asilimia 75 ya mzigo wote wa bajeti ya Afya, huku ugonjwa wa kisukari pekee ukipelekea gharama ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 465 sawa na asilimia 11 ya bajeti yote ya Afya Duniani.
Pia, Dkt. Gwajima ametoa wito kwa Wizara zote kuhakikisha zinaandaa mikakati na mipango shirikishi na jumuishi ya kutekeleza afua mbalimbali za kukinga na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza katika maeneo yao wanayosimamia.
“Nitoe wito kwa Wizara zote kuhakikisha zinaandaa mikakati na mipango ya utekelezaji kwa ajili ya kutekeleza afua mbalimbali za kukinga na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza katika maeneo yao. Mikakati hii ni lazima iwe shirikishi na jumuishi ili kuleta tija kwa Taifa.” Amesema.
Nae Naibu Katibu Mkuu anaeshughulika masuala ya Afya OR TAMISEMI Dkt. Grace Magembe amewashukuru washiriki wote walioandaa maadhimisho hayo na kuweka wazi kuwa, maadhimisho hayo yameleta matokeo chanya kwani watu wameweza kutambua hali zao kupitia huduma za uchunguzi, pia wamepata elimu mbali mbali ikiwemo yakupambana dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.
Pia, Dkt Magembe ameahidi kwenda kusimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri wa Afya ikiwemo Elimu kwa wananchi ya kupambana dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza na elimu juu ya umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya.