Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Busega wamesema watahakikisha wanashiriki na kusimamia vyema Fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19, ambazo zinatumika kujenga vyumba vya madarasa Shule za Sekodari na Shule Shikizi. Hayo yamebainishwa katika baraza la madiwani robo ya kwanza 2021/2022 lililofanyika tarehe 12 Novemba 2021.
Pamoja na mambo mengineyo, madiwani hao wamefurahishwa na mgao wa fedha ambazo zimetolewa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, ambapo Wilaya ya Busega imeweza kupatiwa mgao wa Tshs bilioni 1.9 kwaajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vipatavyo 95.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mhe. Sundi Muniwe amewataka madiwani wote kushiriki ipasavyo katika ujenzi wa vyumba vya madarasa hayo ili kuhakikisha wanafunzi wanapata fursa ya kujiunga na elimu ya kidato ya kwanza ifikapo Januari. “Tushiriki hatua zote kwani sisi ni wasimamizi wa maendeleo maeneo yetu, lengo likiwa ni kufanikisha ukamilikaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa wakati” aliongeza Muniwe.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amewaasa wazazi wenye tabia ya kuwazuia wanafunzi kuhudhuria shule na kueleza kwamba hali hiyo inadumaza ukuaji wa elimu. Zakaria amesema kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wazazi kuwazuia watoto waliofaulu kujiunga na elimu ya sekondari hivyo kushindwa kupata haki yao elimu.
Aidha, Zakaria amesisitiza ushiriki wa madiwani katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kufanikisha ukamilikaji wake kwa wakati. Kwa upande mwingine Zakaria ameipongeza Ofisi ya Halmashauri kwa ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kipindi cha robo ya kwanza kwa kuvuka lengo iliyojiwekea ya asilimia 25 na kufikia asilimia 29, ambapo makusanyo kwa kipindi cha Julai hadi Septemba ni zaidi ya Tshs milioni 588.