Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo
Mratibu wa Kanda maalum inayojumuisha mikoa ya Pwani,Tanga, Kilimanjaro na Arusha na Balozi wa BAKWATA Online Academy,alhaj Abdul SharifZahoro, amewaasa baadhi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kupotosha ama kubeza viongozi wa dini na serikali kuacha tabia hiyo na badala yake watumie vizuri kwa maendeleo yao na kusemea mazuri ya nchi yetu.
Aidha amemshukuru Allah na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zuberi kwa kumteua kushika nafasi hizo za uongozi.
Akizungumza na waandishi wa habari, wilayani Bagamoyo, Sharif alisema mitandao,TEHAMA isigeuzwe eneo la propaganda na kuzusha mabaya.
Alieleza ,endapo vitatumika vizuri vinamnufaisha mtu kwa kuelewa jambo,kuelimisha ama kufundisha na kusemea mema nchi yetu.
Akielezea uteuzi wake, alisema ,Mufti na BAKWATA imetekeleza agizo la Serikali kufuatia waraka wa Serikali kwa taasisi za dini ambapo tarehe 16.4.2020 katika ukurasa wa 3 kipengele cha 3.3 umeagiza kuwapa mafunzo viongozi na watendaji wa Taasisi za dini .
Alibainisha,taasisi za kidini, viongozi wake wakiwemo wa misikiti,masheikh,kata, wilaya,mkoa na mabaraza ya BAKWATA wapate mafunzo ya TEHAMA ni suala muhimu .
Sharif ambae pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa Taasisi ya kidini ya Shakiba Islamic foundation Bagamoyo, aliwahamasisha viongozi hao kusoma mafunzo ya BAKWATA ONLINE ACADEMY ili kuwa na uwezo kusimamia misikiti na mabaraza ya BAKWATA.
“Taasisi zote za dini ya kiislamu zipo chini ya BAKWATA hivyo isitokee taasisi ikadharau hili,lazima watii agizo, wapo baadhi wanaobeza ,Nawaomba isitokee wakadharau,”Kwani BAKWATA hii sio ile ya zamani tumeshuhudia ikisimamia masuala ya kiislamu kwa vitendo”alisisitiza Sharif.
Sharif alifafanua,anatarajia kufanya ziara katika mikoa lengwa kuhamasisha elimu hiyo ili kumuunga mkono Mufti.
Nae katibu Mtendaji wa Taasisi ya kidini ya Shakiba Islamic foundation Bagamoyo, Hassan Kilemba alisema BAKWATA ya Sasa inafaa kupongezwa kwa kazi nzuri inayofanya.
Alielezea kwamba, Sharif anastahili Kutokana na kusimamia masuala ya dini na kushirikiana na waumini wengine kwa kila ari wilayani kwake .