*******************************
Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
Nov 11
WANAFUNZI wa shule ya Sekondari ya Chalinze iliyopo Kitongoji cha Bwilingu Halmashauri ya Chalinze Bagamoyo Pwani, wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa bwalo na adha ya maji.
Hayo yalielezwa na wahitimu wa kidato nne shuleni hapo, mbele ya mgeni rasmi Diwani Nassa Karama aliyemwakilisha Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete.
Salama Idd na Nickson Glorious walieleza kuwa ukosefu wa bwalo inasababisha wanafunzi kukosa eneo la mdahalo, mikutano na masomo ya jioni jambo linalokwamisha juhudi za walimu na wanafunzi.
“Tunakabiliwa na changamoto ya Bwalo linaloweza kuchukua wanafunzi 500, litalotusaidia kwa midahalo, mikutano na masomo nyakati za jioni, hatuna maji pia tunaomba tukarabatiwe vyumba vya madarasa,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kabla ya kumkaribisha Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya shule Diana Magezi, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo George Ndelime amewataka wazazi na walezi wa wahitimu kutofanya sherehe badala yake wawapatie muda wanafunzi wajiandae na mitihani yao.
“Tumeweka makubaliano na wanafunzi wetu kwamba Ijumaa watakuja kwa ajili ya kuandaa vyumba na kupanga meza na viti tayari kwa mitihani yao itayoanza Jumatatu ya Nov 15, msiandae vigodoro waacheni wafannye maandalizi,” alisema
Diana aliwaambia wazazi na walezi wa wanafunzi kuwatunza wahitimu hao, ili kuhakikisha wanaendelea na masomo yao yanayowakabili ngazi mbalimbali, ikiwemo mitihani yao ya kidato cha nne yanayotaraji kufanyika kuanzia Nov 15.
“Wazazi mnapokaa na watoto masaa machache tu mnasema bora aende shule, sasa mnalazimika kukaa nao zaidi ya miezi mitatu tunataka mkatulindie watoto hawa msituletee vibaka mkawe walinzi wazuri kwao,” alisema Diana.
Akizungumza kwenye mahafali hayo, Karama alisema kuwa Halmashauri inaendelea kutekeleza agizo la Waziri Mkuu la kujenga madarasa mawili na ya Wizara mawili ambayo yote yapo kwenye hatua za mwisho, mengine manne ya COVID 19.
“Rais Samia alipokuwa kwenye mkutano wa kimataifa aliwaambia kwamba pesa za COVID sio za kununua Barakoa na chanjo, bali zitakwenda kuboresha elimu kujenga vyumba vingi ili kuwapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu na msongamano darasani, Mama anaupiga mwingi,” alimalizia Karama.