*******************************
KUPATIKANA NA BHANGI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia ABISAI MTEZI [29] Mkazi wa Iyela Jijini Mbeya kwa kosa la kupatikana na dawa za kulevya aina ya Bhangi yenye uzito wa Kilogramu moja.
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 09.11.2021 majira ya saa 03:30 usiku katika msako uliofanyika huko maeneo ya Airport ya zamani iliyopo Kata ya Iyela, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya ambapo alikamatwa akiwa ameficha bhangi hiyo ndani ya nyumba anayoishi. Mtuhumiwa ni muuzaji na mtumiaji wa dawa hizo za kulevya.
KUPATIKANA NA MALI YA WIZI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia ALEX MWAKALUKWA [30] Dereva na Mkazi wa Ndola kwa tuhuma za kupatikana na mali ya wizi bunda nne za kufungia fensi/wigo.
Mtuhumiwa amekamatwa mnamo tarehe 09.11.2021 majira ya saa 08:00 mchana katika msako uliofanyika huko maeneo ya Mapelele, Kata ya Utengule Usongwe, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya.
Mtuhumiwa baada ya kuhojiwa amekiri kuiba mali hiyo kwa YESAYA NGOLOKE [26] Daktari na Mkazi wa Ifisi – Mbalizi.
KUPATIKANA NA MADINI YADHANIWAYO KUWA NI DHAHABU BILA YA KUWA NA LESENI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia SHUAYB YUSUPH ABDULLATIF [42] Mfanyabiashara na Mkazi wa Ilala Bungoni Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kupatikana na madini yanayodhaniwa kuwa ni dhahabu bila kuwa na leseni.
Ni kwamba mnamo tarehe 06.11.2021 majira ya saa 08:32 usiku huko maeneo ya City Pub, Kata ya Iyela, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya Jeshi la Polisi Mkoani hapa kwa kushirikiana na Kikosi kazi cha Taifa cha kupambana na utoroshwaji wa madini nchini, lilipata taarifa za uwepo wa mfanyabiashara wa madini ya dhahabu ambaye anafanya biashara ya kununua madini ya dhahabu bila kufuata utaratibu wa kisheria wa kupitia masoko ya madini nchini.
Jeshi la Polisi liliweka mtego na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa na kifurushi chenye madini ya dhahabu. Mtuhumiwa alihojiwa na kukiri kuwa ana madini mengine nyumbani kwake anapofikia pindi anapofika Mbeya maeneo ya Isyesye. Upekuzi ulifanyika na kufanikiwa kupata madini ya dhahabu vipande 18 vyenye ukubwa tofauti, mzani mmoja wa kupimia madini, jiwe moja la kupimia lenye uzito wa gramu 500 na bakuli 05 za kupimia madini.
Mtuhumiwa alikamatwa na jumla ya vipande 31 vya Dhahabu vyenye uzito wa Gramu 1,177. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika jalada litapelekwa kwa mwanasheria mkuu wa serikali kwa ajili hatua zaidi za kisheria.
MAFANIKIO YA KESI MAHAKAMANI.
Mnamo tarehe 09/11/2021 katika kikao cha mahakama kuu kanda ya Mbeya mbele ya Mhe.Dkt Jaji MONGELLA mshitakiwa SILVANUS NYAULULI [38] Mkazi wa Kijiji cha Limsemi kilichopo Kata ya Ipwani, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali amefungwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mwanaye aitwaye MAVUNO NYAULULI mwenye umri wa mwaka mmoja.
Ni kwamba mnamo tarehe 31.01.2017 majira ya saa 04:00 usiku huko Kijiji cha Limsemi kilichopo Kata ya Ipwani, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya. MAVUNO NYAULULI mwenye umri wa mwaka mmoja aliuawa kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na baba yake mzazi aitwaye SILVANUS NYAULULI [35] ambaye baada ya tukio hilo alikimbia kusikojulikana.
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wasiri lilifanya msako na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa ambaye alikiri kuhusika kwenye tukio hilo. Upelelezi ulifanyika na kufikishwa mahakamani.